“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Ijumaa, Aprili 7, 2023,
IJUMAA KUU
Isa 52:13-53;
Zab 31:2,6,12-13,15-17,25
Ebr 4:14-16, 5:7-9;
Yn 18:1 - 19:42
MTAZAMENI MTU!
Ni Ijumaa kuu, siku ambayo ilikuwa muhimu sana kwa Yesu kwa lengo lake la
kuja ulimwenguni. Maisha yake yote, mafundisho yake yote, kila neno la msamaha
au changamoto hakuna lolote linalo leta maana kama bila msalaba. Na leo
tunaitwa kujiunga na mamilioni ya watu duniani kote kwa kumtazama Mwanakondoo
wa Mungu aliye sulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu.
Kwa maneno ya Pilato. “Mtazameni mtu”, tumtazame Kristo, tukitazama na
kurudi katika unyenyekevu wake wa kuzaliwa katika zizi. Tukikumbuka miaka yake
aliokuwa akikuwa katika hekima na kimo. Tumuone katika unyenyekevu wake,
muamini na kujikabidhi kwa Baba yake, alivyotembea na Mungu katika kila hatua
ya maisha yake. Tazama aliyesali mikononi mwako naiweka roho yangu. Tazama sala
hii aliyoisema wakati akivuta pumzi yake ya mwisho ilivyokuwa, lakini maisha
yake yote yaliojikita ndani ya Baba yake.
Njooni na “tazama aliyesema naona kiu”, tazama aliye ona njaa, kiu, ndani
ya mwili na roho. Hakuja ili kutumikiwa bali kutumikia. Aliosha miguu ya rafiki
zake. Alikula chakula pamoja na wenye dhambi na kuwashika wakoma. Alitoa maisha
yake siku baada ya siku kwa ajili ya watu wake. Na tazama sasa ana sulubishwa
na kukataliwa. Alipigiliwa misumari msalabani na tazama anayatoa maisha yake.
Tazama mfalme wako, ametobolewa na damu inatoka miguuni, tunapiga magoti,
tukitangaza siku ambayo kila mtu atapiga magoti mbele zake. Tumuangalie huyu
mwalimu alivyo haribiwa, na kumuona mfalme wako wa milele, ambaye kwa njia yake
vitu vyote viliumbwa. Mtazame huyu Kuhani mkuu amekaa mbinguni akikuombea
kwasababu ya dhambi zako kama alivyofanya pale msalabani. Mtazame Yesu. Anga
lina giza. Dunia inatetemeka. Miamba ina pasuka. Mwili wake umelala. Ukuu wake
umekuwa tupu kutokana na sababu. Hapa yupo Mfalme wako.
Masomo yana andika maneno saba ya Yesu ya mwisho. Tuya tazame.
1. “Bwana, uwasamehe kwasababu hawajui watendalo”. Akiwa ametundikwa
msalabani akiwa anavumilia ubaya wa wengine, Yesu aliongea maneno ya Msamaha.
Alikiri kwamba hata hawa waliomsulubisha hawakuhusika asilimia zote. Hali hii
ya unenyenyekevu wa Yesu unatambua undani wa huruma yake. Inaonesha kwamba
hakufa akiwa na hasira au chuki, bali kama sadaka safi. Je, upo tayari kusema
maneno haya? Unaweza kuvuta hisia ya watu waliokuumiza ukaita sauti ya Baba
awasamehe wote?
2. “Amini, nakuambia utakuwa nami Paradiso”. Ni zawadi ilikuwa kuu namna
ghani kuwa karibu na mkombozi wa Ulimwengu, kushiriki katika mateso ya Kristo
katika hali halisi. Mwizi huyu alipata zawadi ya kwanza ya kufurahia ukombozi
wa Yesu uliopatikana pale msalabani. Yesu anatupa sisi pia uhakika. Anatupatia
ukombozi. Anatupatia sisi ukombozi huu tukiwa katikati ya mateso na dhambi
zetu. Je, waweza kuisikia sauti yake ikikuita kushiriki katika maisha yake ya
milele?
3. “Mama, tazama mwanao”. Hapa, Yesu kwa kufa msalabani anamkabidhi Mama
yake mzazi kwa Yohane, alimkabidhi kwa kila mmoja wetu. Umoja wetu na Yesu
unatufanya tuwe watu katika familia yake, na hivyo, watoto wa Mama yake
mwenyewe. Je, unamkubali mama wa Yesu kama Mama yako wa kiroho?
4. “Mungu wangu, Mungu wangu, kwanini umeniacha?”. Yesu hakuwa ameachwa
bali aliruhusu kuhisi kuachwa na Baba yake katika hali ya Kibinadamu. Aliruhusu
mwenyewe aweze kutambua na kuelewa madhara ya dhambi. Kwahiyo, anatambua kila
tunachopitia tukiwa katika uchungu. Na yupo nasi katika majaribu akitusaidia
kusonga mbele kwa Imani na kumwamini Baba.
5. “Nina kiu”. Yesu alihisi kiu kwa wakati huo na alihitaji maji ili
kupooza, kupoteza kwake maji mwilini. Lakini zaidi ya hayo, aliona kiu kwa
ukombozi wa roho zetu. Aliona kiu ya kutuita watoto wake. Aliona kiu ya mapendo
yetu. Tuliza kiu yake siku hii ya Ijumaa kuu kwa kumpa mapendo yako.
6. “Baba, mikononi Mwako naiweka roho yangu”. Haya ni maneno ya kujikabidhi
kwa Mungu kabisa. Kujikabidhi maana yake, Mungu ndiye anaye endesha yote. Maana
yake kuachia mapenzi yetu na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatawale. Na ina maana
kwamba Mungu ameahidi kukubali kujikabidhi kwetu na kutuongoza kwenye mpango
wake mkamilifu aliyo tuandalia.
7. “Yametimia” kutimia maana yake nini? Hii ni moja wapo ya maneno ya Yesu
yanayo toa maana kwamba utume wake wa ukombozi wa dunia umetimia. Ina maana
kwamba upendo wake wa sadaka aliyo itoa kwa wote. Kifo chake, tunacho kikumbuka
leo, ni sadaka kamili inayo ondoa dhambi za wote. Ni zawadi iliyoje!
Tumezoea kuiona sadaka hii msalabani. Tunaona zawadi hii daima tunapo
utazama msalaba. Lakini ni vizuri kutambua kwamba kuzoea kwetu misalaba daima
inaweza kutufanya tukashindwa kuona sadaka hii juu ya msalaba. Ni rahisi
kusahau kile ambacho Yesu alitufanyia. Tunaomba tendo hili Takatifu la Kimungu
lizame ndani ya mioyo yetu. Kutambua sadaka ya Yesu alioitoa pale msalabani
itatufanya sisi tupende kama yeye alivyo penda. Itatusadia kuwapenda wale
waliotuumiza na kutuchukia. Upendo wake ni Kamili. Ni wa ukarimu wa kupita
maelezo.
Sala: Bwana, ninajua umeona kiu ya roho yangu. Ulimalizia kile ambacho
ulianzisha kwa kufa juu ya msalaba kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Nisaidie
nitambue upendo wako na kuukubali katika maisha yangu. Ninakushukuru , Bwana
mpendwa kwa zawadi ya damu yako Takatifu, iliomwagika kwa ukombozi wa
Ulimwengu. Bwana, ninakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment