MASOMO YA MISA, JUMAPILI, MACHI 31, 2024
DOMINIKA YA PASAKA
MWANZO:
Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umweniwekea
mkono wako,
maarifa hayo ni ya ajabu, aleluya.
SOMO 1
Mdo. 10:34, 37- 43
Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Jambo
lile ninyi mmelijua, lilionea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya
ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia
mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi
njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu aikuwa pamoja
naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote yaliyotendeka katika nchi ya Wayahudi na
katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku
ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa
wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndiyo sisi, tuliokula na kunywa naye baada ya
ufufuka kwake kutoka kwa wafu. akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa
huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe mhukumu wa wahai na wafu. Huyo manabii wote
humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI.
Zab. 118:1-2, 16-17, 22-23.
K. Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutashangilia na kuifurahia.
Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema
kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele. (K)
Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)
Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la Pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu (K)
SOMO 2
Kol. 3:1-4
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo
juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja
na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi
mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Shangilio
Aleluya Aleluya!
Kristo, Paska wetu amekwisha kutolewa sadaka;
Basi natuifanye karamu katika Bwana!
Aleluya
INJILI
Yn. 20:1-9
Hata siku
ya kwanza ya juma Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza
bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa
Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia,
wamemwondoa Bwana kaburuni, wala hatujui walipomweka. Basi Petro akatoka, na
yule mwanafunzi mwingine , wakashika njia kwenda kaburini wakaenda mbio wote
wawili; na yule mwanafunzi wengine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa
kwanza wa kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda
vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani
ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; ile leso iliyokuwako kichwani
pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezogwazogwa mbali mahali pa peke
yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza
wa kufika kaburini, akaona na kuamini. kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya
kwamba imempasa kufufuka.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment