MASOMO YA MISA, APRILI 1, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 5 LA KWARESIMA
SOMO 1
Eze. 37:21 – 28
Bwana Mungu asema hivi: Tazama, nitawatwaa wana
wa Israeli toka kati ya mataifa walikokwenda, nami nitawakusanya pande zote, na
kuwaleta katika nchi yao wenyewe; nami nitawafanya kuwa taifa moja katika nchi
hiyo, juu ya milima ya Israeli; na mfalme mmoja atakuwa mfalme wao wote; wala
hawatakuwa tena mataifa mawili, wala hawatagawanyikana kuwa falme mbili tena,
hata milele. Wala hawatajitia uchafu tena kwa vinyago vyao, wala kwa vitu vyao
vichukizavyo, wala kwa makosa yao mmojawapo; lakini nitawaokoa, na kuwatoa
katika makao yao yote, ambayo wamefanya dhambi ndani yake, nami nitawatakasa;
basi watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Na mtumishi wangu, Daudi,
atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda
katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda. Nao watakaa katika
nchi niliyompa Yakobo, mtumishi wangu, walimokaa baba zenu; nao watakaa humo,
wao na watoto wao, na watoto wa watoto wao, milele; na Daudi, mtumishi wangu,
atakuwa mkuu wao milele. Tena nitafanya agano la Amani pamoja nao; litakuwa
agano la milele pamoja nao; naami nitaweka na kuwazidisha, na patakatifu pangu
nitapaweka katikati yao milele. Tena maskani yangu itakuwa pamoja nao; nami
nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Na mataifa watajua ya kuwa mimi
ndimi Bwana, mimi niwatakasaye Israeli, patakatifu pangu patakapokuwa katikati
yao milele.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Yer. 31:10 – 13 (K) 10
(K) Bwana anatulinda kama mchungaji alindavyo
kundi lake.
Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa,
Litangazeni visiwani mbali;
Mkaseme: Aliyemtawanya Israeli atamkusanya,
Na kumlinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.
Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo,
Amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko
yeye. (K)
Watakuja na kuimba katika mlima Sayuni.
Wataukimbilia wema wa Bwana,
Nafaka, na divai, na mafuta,
Na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe. (K)
Ndipo bikira atafurahi katika kucheza,
Na vijana na wazee pamoja;
Maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha,
Nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache
huzuni zao. (K)
SHANGILIO
Zab. 95:8 , 9
Leo msifanye migumu mioyo yenu, lakini msikie
sauti yake Bwana.
INJILI
Yn. 11:45 – 57
Wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Maria, na
kuyaona yale aliyoyafanya Yesu, wakamwamini. Lakini wengine wakaenda zao kwa
Mafarisayo, wakawaambia aliyoyafanya.
Basi wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakakusanya
baraza, wakasema, Tunafanya nini? Maana mtu huyu afanya ishara nyingi.
Tukimwacha hivi, watu wote watamwamini; na Warumi watakuja watamuondolea mahali
petu na taifa letu. Mtu mmoja miongoni mwao, Kayafa, aliyekuwa Kuhani Mkuu
mwaka ule, akawaambia, Ninyi hamjui neno lolote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa
mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala lisiangamie taifa zima. Na neno hilo yeye
hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule,
alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo, wala si kwa ajili ya
taifa hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika,
ili waawe wamoja. Basi tangu siku ile walifanya shauri la kumwua.
Kwa hiyo Yesu hakutembea tena kwa wazi katikati
ya Wayahudi; bali alitoka huko, akaenda mahali karibu na jangwa, mpaka mji
uitwao Efraimu; akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
Na Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; na wengi
wakakwea toka mashambani kwenda Yerusalemu kabla ya Pasaka, ili wajitakase.
Basi wao wakamtafuta Yesu, wakasemezana hali wamesimama hekaluni, Mwaonaje?
Haji kabisa sikukuu hii? Na wakuu wa makuhani wa Mafarisayo walikuwa wametoa
amri ya kwamba mtu akijua alipo, alete habari, ili wapate kumkamata.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment