MASOMO YA MISA, MACHI 18, 2024
JUMATATU, JUMA LA 5 LA KWARESIMA
SOMO 1
Dan.13:41-62
Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu, akikaa
Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na
mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao
sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na
nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa
ni mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili
miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena,
ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala
watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na
wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka
kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili
kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka
tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho
yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa walipongoja
wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na
wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa
na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi
akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya
bustani ili nioge . Mara wale wajakazi walipokwishas kutoka, wale wazee wawili
waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa
asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali na
ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja
nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema,
Nimesongwa pande zote, maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda
siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali niangukie katika mikono yenu na
kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa
sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao
akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani
waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili
waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadith yao nao
watumishi wakaona aibu kabisa, kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna
hiyo wakati wowote.
Ikawa kesho yake watu walipokusanyika kwa
Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya
Susana la kumfisha. Wakasema mbele ya watu, "Mwiteni Susana binti Helkia,
mkewe Yoakim, aje hapa". Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba
yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote. Naye huyo Susana alikuwa
mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe
uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake. Kwa hiyo rafiki zake na
wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati
ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi,
akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu. Wale wazee
wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja
na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu
wajakazi. Kisha kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala
naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliona ubaya huo,
tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza
kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango akaepuka.
Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo
basi, tunashuhudu. Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na
waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee
Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe
wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa kufa; walakini
sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.
Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo,
alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja, jina
lake Danieli; naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari
ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, Maneno hayo
uyasemayo, maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli,
mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika
ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo.
Basi watu wote walirejea kwa haraka, nao wale
wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu
amekupa wewe heshima yam zee. Hapo Danieli aliwaambia, Watu hawa wawili
watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja wao
akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia,
ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na
kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, Asiye na hatia, mwenye haki, usimwue.
Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona
wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi. Danieli akasema, Hakika
umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sas hivi malaika wa Mungu
amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. akamtenga huyo tena, akaamuru
kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa Yuda, uzuri
umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia
binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza
kuustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani ulipowaona
wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, Hakika wewe
nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu
tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize nyote
wawili.
Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa
nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee
wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani
mwao wenyewe. Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa
ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia
aliokolewa siku ile.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23 (K) 4
(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati aya bonde la uvuli wa
mauti
Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja
nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe change kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zinanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 6:64, 69
Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima,
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
INJILI
Yn. 8:12-20
Yesu aliwaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya
ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya
uzima.
Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia
mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.
Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa
ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka
na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako. Ninyi mwahukumu kwa
kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu. Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni
kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi nay eye aliyenipeleka. Tena
katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. Mimi
ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.
Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu
akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui kama mngalinijijua mimi,
mngalimjua na Baba yangu.
Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha
hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu
saa yake ilikuwa haijaja bado.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment