MASOMO YA MISA, APRILI 25, 2023
JUMANNE, JUMA LA 3 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo 4:32-37
Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo
mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho
nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume
wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa
juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa
sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya
vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa
kadiri ya alivyohitaji. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake,
Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba
akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 93:1-2, 5
(K)Bwana ametamalaki, amejivika adhama.
Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu. (K)
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)
Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee Bwana, milele na milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Bwana asema: mimi ndimi mchungaji mwema; Nao
walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn 3:7-15
Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa
mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui
unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa
Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? Yesu akajibu,
akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin,
amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona
twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. Ikiwa nimewaambia mambo ya
duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala
hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana
wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana
wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika
yeye.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment