MASOMO YA MISA, APRILI 4, 2023
JUMANNE YA JUMA KUU
SOMO 1
Isa
49:1-6
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu,
enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo
la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama
upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa
mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha; akaniambia; Wewe u mtumishi
wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha
bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana,
na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba
tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli
wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya
Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana
wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa
Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa
wokovu wangu hata miisho ya dunia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 71:1-6, 15, 17
(K)Kinywa changu kitasimulia wokovu wako.
Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe. (K)
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)
Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu. (K)
Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako
Mchana kutwa;
maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. (K)
INJILI
Yn 13:21-33, 36-38
Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika
rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti.
Wanafunzi wakatazamana, huku wakiona shaka ni nani amtajaye. Na palikuwapo
mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda. Basi
Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye? Basi yeye,
hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani? Basi Yesu akajibu,
Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa
akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Na baada ya hilo tonge Shetani
alimwingia. Basi Yesu akamwambia, Uyatendayo yatende upesi. Wala hakuna mtu
katika wale walioketi chakulani aliyeijua sababu ya kumwambia hivyo. Kwa maana
wengine walidhania, kwa kuwa Yuda huchukua mfuko, ya kwamba Yesu alimwambia
kama, Nunua mnavyovihitaji kwa sikukuu; au kwamba awape maskini kitu. Basi
huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku.
Basi huyo alipokwisha kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu,
naye Mungu ametukuzwa ndani yake. Mungu naye atamtukuza ndani ya nafsi yake;
naye atamtukuza mara. Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi;
mtanitafuta; na kama vile nilivyowaambia Wayahudi ya kwamba, Mimi niendako
ninyi hamwezi kuja; kadhalika sasa nawaambia ninyi. Simoni Petro akamwambia,
Bwana, unakwendapi? Yesu akamjibu, Niendako huwezi kunifuata sasa; lakini
utanifuata baadaye. Petro akamwambia, Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata
sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako. Yesu akamjibu, Je! Wewe utautoa
uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin, nakuambia, Jimbi hatawika hata wewe
utakapokuwa umenikana mara tatu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment