MASOMO YA MISA, APRILI 03, 2023
JUMATATU YA JUMA KUU
SOMO 1
Isa 42:1-7
Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule
wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye
atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya
isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao
moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa,
hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mungu Bwana
anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao
yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao
ndani yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na
kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya
vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika
nyumba ya kufungwa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 27:1-3, 13-14
(K)Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)
Watenda mabaya waliponikaribia,
Wanile nyama yangu,
Watesi wangu na adui zangu,
Walijikwaa wakaanguka. (K)
Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea,
Hata hapo nitatumaini. (K)
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari,
Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)
INJILI
Yn 12:1-11
Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika
Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu Basi
wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo
wa wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu
ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa
nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. Basi Yuda Iskariote,
mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, Mbona
marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini? Naye aliyasema
hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika
mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku
ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi
hamnami sikuzote. Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye
yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye
Yesu alimfufua katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua
Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga,
wakamwamini Yesu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment