Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUKUTANA NA YESU MFUFUKA KATIKA MAISHA YETU!


“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumapili, Aprili 23, 2023 
Juma la 3 la Pasaka

Mdo 2: 14, 22-33;
Zab 15: 1-2, 5, 7-11;
1 Pet 1: 17-21;
Lk 24: 13-35.


KUKUTANA NA YESU MFUFUKA KATIKA MAISHA YETU!

Katika Asia ndogo, mwaka 80-90 AD, karibia mashuhuda wote wa Yesu mfufuka walikuwa wamesha toweka. Wakristo (wa kizazi cha tatu) wanajiuliza wenyewe: je, inawezekana sisi kukutana na Bwana? Inawezekanaje, kutoa ushuhuda kwamba yupo hai wakati sisi hatukumuona kwa macho, hatukumshika kwa mikono yetu, na wala hatukukaa mezani pamoja naye? Je sisi tunaongozwa tu kuamini kile walicho amini na kutuambia sisi? Wakristo wana tamani kumuona Yesu.

Injili ya Luka kuhusu habari ya Emaus huenda ilikuwa ndio uvuvio wa majibu na matarajio ya Wakristo hawa. Mmoja wa wawafuasi aliitwa Cleopa (mtu ambaye alijulikana sana wakati wa Kanisa la mwanzo, kwasababu alikuwa ndugu wa Yosefu, Yosefu “Baba” mlishi wa Yesu) na mwingine hajatajwa jina. Luka anaweza kuwa amefanya hivyo, kumwalika msomaji kuwa mfuasi wa pili. Mwaliko ni wito wa kutembea na Cleopa katika njia ya kumtambua Yesu mfufuka, ili kukusanyika pale ambapo wawili wamekusanyika kwa jina lake. 

Hawa wafuasi wawili wana huzuni kwasababu wameona maanguko ya mtarajio yao. Walimtazamia Masiha wa utukufu, mkuu na mfalme lakini wamejikuta wakipoteza. Marabi walifundisha kwamba, Masiha ataishi na kuongoza kwa muda wa miaka elfu moja, na tazama sasa Yesu amekufa. Walikata tamaa na kujikuta wakiona ukweli kwamba ulimwengu uliotangazwa na Yesu haukutimia. Bila Imani ya ufufuko, walioshindwa wameshindwa, maisha mwisho wake kifo, na maisha hayana maana. 

Hawa wafuasi wawili wa Emausi hawakuwa na shaka kwamba mawazo yao kuhusu Masiha yalikuwa sio sahihi. Walikuwa wamefungwa katika tamaduni na mapokeo. Walikuwa wamejifungia na kushindwa kufahamu mapya ya Mungu. Yesu hamwachi mtu ambaye anaamua kuchagua mwenyewe kwenda katika njia ya huzuni. Yeye huwa anakuwa pembeni na kuwa msindikizaji. Kutokea kwa Yesu kwa wanafunzi wake inashangaza sana. Yesu “anawafafanulia yote yaliosemwa kuhusu yeye katika Maandiko Matakatifu”. Kwa njia hiyo hawa wafuasi walitambua kwamba huyu mtu ana uelewa na hekima ya hali ya juu, na hivyo walimwalika akae pamoja nao. Yesu alikaa nao na kula nao chakula mezani nyumbani kwao. Walivyokuwa mezani “alichukua mkate, na kuubariki na kuumega na kuwapa vipande”. Macho yao yalifunguliwa na kumtambua Yesu mfufuka. Wale wafuasi baada ya kumtambua Yesu, walikimbia na kwenda kuwapasha habari na kutangaza kwamba “Bwana amefufuka kweli kweli”.

Habari ya wafuasi wa Emausi inarudiwa kila siku katika Liturjia ya Ekaristi (Misa Takatifu). Inaanza kwa kuingia kwa padre, alafu Liturjia ya neno la Mungu na homilia, na mwishowe, “kuumega mkate”. Ni katika wakati wa Ekaristi takatifu macho yetu yanafumbuliwa tunatambua kwamba Yesu mfufuka yupo kati yetu. Bila neno hatuwezi kuja kumtambua Bwana, hatuwezi kumtambua Yesu katika Ekaristi Takatifu. Wakati misa inaisha tunamaliza na wimbo wa mwisho na hatimaye tunaondoka na furaha, kwenda kushirikisha furaha ya Yesu mfufuka. 

Misa takatifu ni safari yetu ya Emmaus. Tunapaswa kujikita wenyewe katika kumuona Yesu, na kumtambua na kumwabudu. Tunapaswa kutambua uwepo wa Yesu mfufuka kati yetu. Yupo nasi hapa sasa, anatupenda sisi, anaongea na sisi, na anatuita tumpende yeye. Mtafute na msikilize sauti yake. Tutashangaa ni kwa jinsi ghani Bwana mfufuka atakavyo tufanya tutembee naye katika Maandiko Matakatifu, na kujifunua mwenyewe na kuleta furaha katika huzuni yetu na katika mioyo yetu iliokata tamaa. 

Sala: Bwana, ninakushukuru kwa kunipenda mimi sana kiasi kwamba upo na mimi daima. Nipe macho ya Imani niweze kukutana nawe katika Maandiko Matakatifu na kukuona wewe ukiwa ndani ya Ekaristi Takatifu. Ninaomba niweze kutambua uwepo wako katika mambo ya kawaida yanayo tokea katika maisha yangu. Ninakupenda Bwana wangu. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment