“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumanne, Februari 27, 2024
Juma la 2 la Kwaresima
Isa 1:10, 16-20;
Zab 50:8-9,16-17,21,23;
Mt 23:1-12
UNYENYEKEVU MBEGU YA KIMUNGU!
Leo nabii Isaya anawaambia wana Waisraeli wafanye uchaguzi. Wajioneshe
wenyewe na waache kutenda maovu. Kwaresima ni kipindi cha neema kubwa, ni muda
ambao tunapaswa kutafakari ni wapi tulipo kosea na kujaribu kurekebisha. Kama
nimechukua fedha isio halali niangalie jinsi ya kurudisha. Kama nilikuwa mtu wa
kuapa, niache na kubadilika. Katika hali yeyote, napaswa kufanya kitu. Naweza
kuhitaji sakramenti ya kitubio au kutafuta upatanisho na mtu ambaye nilimuumiza
au aliyeniumiza.
Yesu anatupa somo zuri sana katika Injili. Anatutaka sisi tuweze kutukuka!
Anatutaka sisi tujulikane na wengine. Anataka mwanga wetu mzuri uangaze watu
waweze kuuona na kwa mwanga huo waweze kufanya mabadiliko. Lakini anapenda hili
lifanyike katika kweli sio katika hali ya kudanganya. Anataka ukweli wa “mimi”
uangaze. Nao ni unyenyekevu. Unyenyekevu ni kuwa mnyofu na mwaminifu. Na wakati
watu watakapo ona hali hii ndani yetu, watavutwa. Sio sana katika hali ya
kidunia bali katika hali ya kibinadamu. Hawata tuangalia na kuwa na wivu bali,
watatuangalia na kuona ukweli wenyewe na kuufurahia, kuutamani na kutaka
kuuishi. Unyenyekevu unakusaidia ukweli kamili kuhusu wewe uweze kungaa. Na
wewe ukiwa katika kweli unakuwa ndiye mtu mwingine ambaye wengine wanataka kukutana
naye.
Sala: Bwana, naomba unifanye niwe mnyenyekevu. Nakuomba niweze kuwa
mwaminifu na mkweli kwa jinsi nilivyo. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment