MASOMO YA MISA, FEBRUARI 23, 2026
JUMATATU, JUMA LA 1 LA KWARESIMA
SOMO 1
Law. 19:1-2, 11-18
Bwana akanena na Musa, akamwambia, Nena na
mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi
Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.
Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo.
Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi
Bwana. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake
aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala
usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Msitende
yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye
nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huko na huko katikati ya
watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; Mimi
ndimi Bwana. Usimchukie ndigu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani
yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na
kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako nafsi yako; Mimi
ndimi Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:7-9, 14 (K) Yn. 6:64
(K) Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.
Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima. (K)
Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru. (K)
Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele,
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa. (K)
Maneno ya kinywa changu,
Na mawazo ya moyo wangu,
Yapate kibali mbele zake, Ee Bwana,
Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)
SHANGILIO
Zab. 51:1-10, 12
Ee Mungu, uniumbie mioyo yenu;
Unirudishie
furaha ya wokovu wako.
INJILI
Mt. 25:31-46
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo atakapokuja
Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye,
ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika
mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;
atawaweka kodnoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.
Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake
wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliowekewa tayari
tangu kuubwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na
kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika;
nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.
Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana,
ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni
lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Na Mfalme
atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao
ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa
kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa
tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula;
nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi,
msinivike; nalikuwa mgonjwa na kifungoni, msije kunitazama.
Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini
tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au
u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri
msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao
watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda
katika uzima wa milele.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment