MASOMO YA MISA, MACHI 23, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 4 LA KWARESIMA
SOMO 1
Kut. 32:7-14
Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka kwa maana
watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka
upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia kuyeyusha, wakaiabudu na
kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa
katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na
tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake
juu yao, niwaangamize; nami ninakufanya wewe uwe taifa kuu.
Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema,
Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya
Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena,
wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ilia pate kuwaua milimani, na kuwaondoa
watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio
nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako,
ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa
nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao
watairithi milele. Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda
watu wake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 106:19-23 (K) 4
(K) Ee Bwana unikumbuke mimi,
kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)
Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri. (K)
Akasema ya kuwa atawaangamiza,
Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali palipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)
SHANGILIO
Mt. 4:17
Tubuni, asema Bwana, kwa maana ufalme wa
mbinguni umekaribia.
INJILI
Yn. 5:31-47
Yesu aliwambia Wayahudi: Mimi nikijishuhudia
mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayeshuhudia; nami najua ya
kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohane, naye
akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini
ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa,
nanyi mlipenda kuishangilia nuru yake kwa muda.
Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko
ule wa Yohane; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo
zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba
aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura
yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi
hammwamini yule aliyetumwa na yeye.
Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani
kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.
Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa
wanadamu. Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu.
Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa
jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.
Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu
ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?
Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa,
mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa
sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake,
mtayaamini wapi maneno yangu?
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment