MASOMO YA MISA, MACHI 22, 2023
JUMATANO, JUMA LA 4 LA KWARESIMA
SOMO 1
Isa. 49:8-15
Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika
nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe
agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa
ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza,
Jionyesheni.
Watajilisha katika njia, na juu ya majabali
watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala
jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za
maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu
zitatukuzwa zote.
Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama,
hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya sinimu.
Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; kwa
kuwa Bwana amewafariji watu wake, naye atawahurumia watu wake walioteswa.
Bali Sayuni alisema, Yehova ameniacha, Bwana
amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie
mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:8-9, 13-14, 17-18 (K)
(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.
Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Ni mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)
Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)
SHANGILIO
Mt. 4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno
litokalo katika kinywa cha Mungu.
INJILI
Yn. 5:17-30
Yesu aliwajibu Wayahudi: Baba yangu anatenda
kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi
kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita
Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu.
Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin,
nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba
analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.
Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na
kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonyesha ili ninyi mpate kustaajabu. Maana
kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana ahuisha wale
awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu yeyote, bali amempa Mwana hukumu yote, ili
watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana
hamheshimu Baba aliyempeleka.
Amin, amin, nawaambia, yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia,
Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale
waisikiao watakuwa hai.
Maana kam avile Baba alivyo na uzima nafsini
mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa
amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo;
kwa maana sasa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda
mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo
ndivyo nihukumuvyo na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi
yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment