MASOMO YA MISA, MACHI 15, 2023
JUMATANO, JUMA LA 3 LA KWARESIMA
SOMO 1
Kumb. 4:1, 5-9
Musa aliwaambia makutano: Ee Israeli,
zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mmzitende; mpate kuishi na
kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu.
Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile
vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi
mwmingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima
yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao
watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko
taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu,
alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu
zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho
yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako,
yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako
na watoto wa watoto wako.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 147:12-13, 15-16, 19-20 (K) 12
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako. (K)
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,
Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)
Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)
SHANGILIO
Mbegu neno la Mungu, mpanzi lakini ni Kristu;
Yeyote ampataye, ataishi milele.
Yeyote ampataye, ataishi milele.
INJILI
Mt. 5:17-19
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani kuwa
nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa
maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala
nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. Basi mtu yeyote
atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo,
ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na
kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment