MASOMO YA MISA, FEBRUARI 19, 2026
ALHAMISI BAADA YA MAJIVU
SOMO 1
Kum. 30:15-20
Musa aliwaambia watu akisema: Aangalia,
nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi
nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na
kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka;
Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini
moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu
miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia;
hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yoradani, uingie
kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea
mbele yako uzima na mauti Baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe
na uzao wako; kupenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana
naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika
nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 1:1-4, 6 (K) Zab. 39:5
(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini
lake.
Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)
Naye atakuwa kama mti ulipopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SHANGILIO
Zab. 130:5
Nimemgnoja Bwana, roho yangu imengoja, na neno
lake nimelitumaini. Nafsi yangu inamngoja Bwana, kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
naam, walinzi waingojao asubuhi.
INJILI
Lk. 9:22-25
Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba
imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee na wakuu wa
makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.
Akawaambia wote, Mtu yeyote akitaka kunifuata,
na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu
atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake
kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata
ulimwengu wote, kama akijiangamiza, na kujipoteza mwenyewe?
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment