MASOMO YA MISA, MACHI 6, 2023
JUMATATU, JUMA LA 2 LA KWARESIMA
SOMO 1
Dan. 9:4 – 10
Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye
maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi,
tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo
yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa
jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote
wa nchi.
Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna
haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na
kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote
ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna
haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu
tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa
tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria
zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 79:8 – 9, 11, 13 (K) 103:10
(K) Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.
Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumedhilika sana. (K)
Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)
Kuugua kwake aliyefungwa na kuingia mbele zako.
Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako.
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho
yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)
SHANGILIO
Mt. 4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno
litokalo katika kinywa cha Mungu.
INJILI
Lk. 6:36:38
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Iweni na huruma,
kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu,
nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu kitu, nanyi
mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika,
ndicho watu watakachowapa vifruani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho
ndicho mtakachopimiwa.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment