Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

JUMA LA TATU LA KWARESMA - NJIA YA MSALABA


Kabla ya kila kituo: 
K: Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru;
W: Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.

Baada ya kila kituo:
'Baba Yetu, 'Salamu Maria' na 'Atukuzwe Baba',
K: Ee Bwana utuhurumie! W: Utuhurumie!
K: Roho za waamini marehemu, wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa amani. W: Amina



SALA YA KUFUNGUA
Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake bustanini Gethsemane, akawaambia, "Kaeni hapa nami niendc pale mbele kusali". Akawachukua Petra na wana wawil wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko Hapo akawaambia, “'Nina huzuni kubwa moyoni hate karibu ya kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami". Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akasali, "Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki cha mateso kinipitie; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe". (Mt 26:36-39).

Mungu Baba Mwenyezi, pokea sala yetu ya shukrani tuitoayo kwa Mwanao mpendwa, Mwokozi na Bwana wetu. Tunapoyakumbuka mateso yake matakatifu, peleka Roho wako Mtakatifu mioyoni mwetu ili tusalipo au tufanyapo kazi, yote tuyafanye tumeunganika na Kristo Mkombozi wetu, anayeishi na kutawala daima na milele. Amina. 

KITUO CHA KWANZA - YESU ANAHUKUMIWA AFE
P: Kuhani Mkuu akamwuliza tena. "Je, wewe ndiye Masiha, Mwana wa Mungu Mtukufu?” Yesu akajibu, "Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni”. Hapo Kuhani Mkuu akararua joho lake, akasema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake! Ninyi mwaonaje?” Wote wakamua kwamba anastahili kuuawa. (Mk 14:61-64).

W: Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, juu ya Bwana na juu ya Masiha wake, Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako na miisho ya dunia kuwa milki yako. (Zab 2:7-8).

Tuombe: Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia kwa kutamka kuwa wewe ni Mwana wa Mungu umehukumiwa kufa bila kosa. Tufanye tusikuhukumu mara nyingine kufa kwa dhambi zetu bali kutokana na kifo chako tujaliwe ujasiri wa kukukiri wewe unayekaa upande wa Mwenye-enzi na kutawala daima na milele. Amina

KITUO CHA PILI - YESU ANAPOKEA MSALABA
P. Pilato akawaambia Wayahudi, "Tazameni mfalme wenu!' Wao wakapaaza sauti: "Mwondoe! Mwondoe! Msulibishe!' Pilato akawauliza, 'Je, nimsulibishe Mfalme wenu?' Makuhani wakuu wakajibu, "Sisi hatuna Mfalme isipokuwa Kaisari!” Basi, hapo Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulibiwe. Basi, wakamchukua Yesu. Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo, ‘Fuvu la Kichwa’ (Kwa Kiebrania Golgota) (Yn 19:14-17).

W. Ni nani aliyesadiki habari tuliyoisikia? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo Na kama mzizi katika nchi kavu. Yeye hana umbo wala uzuri Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu. Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu (Isa 53:1-3).

Tuombe: Baba wa mbinguni, kwa kumkiri Mwanao Yesu Kristo, kaka na dada zake wanabebeshwa msalaba wa mateso. Uwe nao wanaodhulumiwa na kudhalilishwa kwa ajili ya jina la Kristo, Bwana wetu. Amina.

KITUO CHA TATU - YESU ANAANGUKA MARA YA KWANZA
P. 'Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi. Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi, watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu. ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. Kumbukeni niltyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko Bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia. (Yn 15:18-20).

W. Kwani mavazi yako kuwa mekundu, Na nguo zako kama za mtu akanyagaye zabibu? Nilikanyaga shinikizoni peke yangu; Wala katika watu hakuwapo mtu pamoja nami; Naam, naliwakanyaga kwa hasira yangu, Naliwaponda kwa ghadhabu yangu; Na mavazi yangu yametiwa madoa kwa damu yao, Nami nimezichafua nguo zangu zote. Nikatazama, wala hakuna wa kunisaidia; Nikashangaa kwa kuwa hakuna mwenye kutegemeza; Basi mkono wangu mwenyewe uliniletea wokovu, Ghadhabu yangu ndiyo iliyonitegemeza (Isa 63:2,3,5).

Tuombe: Tunakushukuru Yesu kwa kutuchagua kuendeleza kazi ya ukombozi wa binadamu. Tukianguka ututie shime tuamke, tusimame mara kutumikia watu wote hata kama dunia inatuchukia. Amina

KITUO CHA NNE - YESU ANAKUTANA NA MAMA YAKA
P: Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya Mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalena. Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: ‘Mama, Tazama, huyo ndiye mwanao’. Halafu akamwambia yule mwanafunzi: Tazama, huyo ndiye mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake. (Yn 19:25-27).

W. Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, Wala hakuona huruma; Ameziangusha ngome za binti Yuda Katika ghadhabu yake; Amezibomoa hata nchi Ameunajisi ufalme wa wakuu wake.
Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nani, Ee Binti Yerusalemu? Nikusawazishe na nani, nipate kukufariji, Ee Bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya? (Omb. 2:13).

Tuombe: Mama Maria, mateso ya Mwanao ndio upanga wa uchungu uliotoboa moyo wako kama Simeoni alivyotabiri. Ewe uliyetolewa uwe mama yetu, tusaidie tutambue kwa njia ya imani maana ya matatizo magumu katika maisha. Amina

KITUO CHA TANO - SIMONI WA KIRENE ANABEBESHWA MSALABA AUCHUKUE NYUMA YA YASU
P: Walipokuwa wanampeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye Simoni wa Kirene, aliyekuwa anatoka mashambani. Basi, walimkamata, wakamtwisha ule msalaba auchukue nyuma yake Yesu. Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgota, maana yake "Mahali pa Fuvu la Kichwa" (Lk 23:26; Mk 15:21).

W. Kwa sauti yangu nitamlilia Bwana, kwa sauti yangu nitamwomba Bwana dua. Nitafunua mbele zaka malalamiko yangu, shida yangu nitaitangaza mbele zake. Nilipozimia roho yangu uliyajua mapito yangu; Katika njia niendayo wamenifichia mtego. Utazama mkono wa kuume ukaone, kwa maana sina mtu anijuaye. Makimbilio yamenipolea, hakuna wa kunitunza roho. Bwana nimekuita nikasema, Ndiwe kimbilio langu, Fungu langu katka nchi ya walio hai (Zab 141:1-5)

Tuombe: Bwana Yesu, tunakutana na watu wanaoteseka ambao umewaweka katika njia tunayopita. Tufundishe kuwaonea huruma na tuwe tayari kuchukua pamoja nao msalaba wao. Amina

KITUO CHA SITA - VERONIKA ANAUPANGUSA USO WA YESU
P. Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme: "Bwana, lini tulikuona mwenye njaa tukakupa chakula, au ukiwa na kiu tukakunywesha maji? Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha au bila nguo tukakuvika? Lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukaja kukutazama?” Mfalme atawajibu: “Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi" (Mt 25:37-40).

W. Walakini rafiki aliye amini ndiye ngome; naye aliyempata amepata tunu. Hakuna badala ya rafiki amini, wala uzuri wake hauna bei. Rafiki amini ni kifunga uzima; naye amchaye Mungu atampata. Mcha Mungu hunyoosha urafiki wake, kwa maana alivyo yeye mwenyewe, ndivyo alivyo na jirani yake 
(YbS 6:14-17).

Tuombe: Yesu, tufanye tuone uso wako ndani ya wanaoteseka. Katika mateso utufundishe upendo, utufundishe upendo hasa katika mateso. Amina

KITUO CHA SABA - YESU ANAANGUKA MARA YA PILI
P: Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhani ya kuwa amepigwa. Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Basi alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yatu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote (Isa 53:4-6).

W. Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana kondoo apelekwaye machinjioni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake;
Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeyasimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu (Isa 53:7-8).

Tuombe: Ee Bwana Yesu, kuanguka kwako chini ya uzito wa msalaba ni kielelezo cha kuanguka kwetu chini ya uzito wa dhambi na makosa. Angaza dhamiri zetu tuone udhaifu wetu. Tupe nguvu ya kutubu kwa dhati tusirudie tena dhambi. Amina

KITUO CHA NANE - AKINA MAMA WANAMLILIA YESU
P. Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao vakiwamo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. Yesu akawageukia, akasema, "Enyi akina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu (Lk 23:27-28).

W. Je si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame kama kuna majonzi yoyote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, ambayo Bwana amenihuzunisha kwa hayo. Siku za hasira yake iwakayo. Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; kwa kuwa mfariji yu mbali nami, ambayo ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa poke yao, kwa sababu huyo adui ameshinda (Omb 1:12-16).

Tuombe: Bwana Yesu, hawa wanawake wa Yerusalemu waliodondosha machozi ya huruma walipokuona njiani kwenda Kalvari umepigwa, umechubuliwa, umetobolewa na miiba. Ongeza imani yangu ili niweze kukuona katika ndugu yangu aliyepigwa kwa maneno yangu mabaya, aliyechubuliwa kwa wivu wangu, aliyetobolewa kwa kumkosea haki. Amina

KITUO CHA TISA - YESU ANAANGUKA MARA YA TATU
P. Nafsi yangu imeambatana na mavumbi, unihuisha sawasawa na neno lako. Nalizisimulia njia zangu ukanijibu, unifundisha amri zako. Unifahamisha njia ya mausia yako, nami nitayatafakari maajabu yako. Nafsi yangu imeyeyuka kwa uzito, unitie nguvu sawasawa na neno lako (Zab 119: 25-28). 

W. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Watanda mabaya waliponikaribia, wanile nyama yangu, watesi wangu na adui zangu, walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami. Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, hata hapo nitatumaini (Zab 27:1-3).

Tuombe: Ee Yesu, kwa kuzidi kudhoofika kwa mateso unaanguka mara ya tatu chini ya msalaba. Tunakuomba, gusa kwa neema yako dhamiri zatu tupata kujua kweli ubaya wa dhambi ulizokuja kuondoa kwa mateso na ufufuko wako. Amina

KITUO CHA KUMI - YESU ANAVULIWA NGUO
P. Nao askari walipomsulibisha Yesu wakampa kunywa divai iliyochanganywa na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa... Walitwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana, ‘tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani’. Ili litimie andiko lile linenalo, waligawana nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari (Mt 27:34; Yn 19:23-24).

W. Laumu imenivunja moyo, nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;
Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu. Wakanipa uchungu kuwa chakula changu: nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. Wao wananitazama na kunikodolea macho. Wanagawanya nguo zangu na vazi langu wanalipigia kura. Nawe Bwana. usiwe mbali, Ee nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia (Zab 69:20-21; 22:17-19).

Tuombe: Bwana unavuliwa nguo na kutoneshwa madonda yako. Tupe, tunakuomba, ujasiri wa kuvua cho chote kisichostahili kuvaa juu ya ile nguo nyeupe ya ubatizo ambayo ulitustahilia kwa gharama kubwa namna hiyo. Amina

KITUO CHA KUMI NA MOJA - YESU ANASULUBISHWA MSALABANI
P. Walipofika mahali palipoitwa, "Fuvu la Kichwa", ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili mmoja upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto. Yesu akasema, ‘Baba uwasamehe kwani hawajui wanalofanya’. Yesu akalia kwa sauti kubwa akisema, "Eloi Eloi, lema Sabakthani?" maana yake, ‘Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" (Lk 23:33-34; Mk 15:34).

W. Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, na maneno ya kuugua kwangu? Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu, na wakati wa usiku lakini sipati raha. Lakini mimi ni mdudu wala si mtu. Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema amemtegemea Bwana; na amponye, na amwokoe sasa, maana amependwa naye. Nguvu zangu zimekauka kama gae, Ulimi wangu waambatana na taya zangu; unaniweka katika mavumbi ya mauti. Kwa maana mbwa wamenizunguka; Kusanyiko la waovu wamenisonga; wamenitoboa mikono na miguu. Naweza kuihesabu mifupa yangu yote (Zab 22:1-2; 4:6-8,15-17).

Tuombe: Bwana na mkombozi, umetuambia kuwa sharti tukubali kusulubiwa kama tunataka kupata ufufuko. Tusaidie tufurahie mateso yanayotokana na kutimiza wajibu wetu wa kila siku, tuyaone kama njia kuu ya kuufiki ufufuko wetu. Amina

KITUO CHA KUMI NA MBILI - YESU ANAKUFA MSALABANI
P. Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaivamia nchi yote mpaka saa tisa, na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi nwako naiweka roho yangu”. Alipokwisha kusema hayo, akatoa roho. Jemadari na wale waliokuwa wakimchunga Yesu walipoona mtetemeko wa ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “kweli mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu” (Lk 23:44-46; Mt 27:54).

W. Kabila langu, Nimekutendea nini? au kwa jambo gani nimekusikitisha? Nijibu !
1.  Mimi nimekukomboa kutoka nchi ya Misri, nawe ukamtengenezea mkombozi wako msalaba.
2. Mimi nimewapiga mijeledi Wamisri kwa ajili yako, nakamtoa mkombozi wako apigwe mijeledi.
3. Mimi nimeifunua bahari ya Sham mbele yako, nawe ukaufunua ubavu wangu kwa mkuki.
4. Mimi nimekulisha mana na maji jangwani, nawe ukaninywesha nyongo na siki.
5. Mimi nimewapiga wafalme wa Kanaani kwa ajili yako, nawe ukanipiga kichwa changu kwa mwanzi.
6. Mimi nimekutukuza na kukuinua juu ya mataifa, nawe ukanitundika katika mti wa msalaba.
Kabila langu, Nimekutendea nini? au kwa jambo gani nimekusikitisha? Nijibu ! 
(Kutoka “Mashutumu ya Ijumaa Kuu, “Kabila langu”)

Tuombe: Bwana Yesu, tunatangaza kifo chako mpaka utakapokuja. Tunaomba tangazo hili liwafikie watu wote wasiokujua. Wote wakukiri wewe uliye hekalu jipya la kumwabudia Mungu. Wale wakutafutao katika kivuli wajalie Roho wako, waweze kukukiri kama wale wapagani “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu”. Amina

KITUO CHA KUMI NA TATU - YESU ANASHUSHWA MSALABANI
P: Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja miguu. Lakini askari mmoja akamtoboa ubavuni kwa mkuki na mara ikatoka damu na maji. Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Arimataya, alimuomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. Basi Pilato akaamuru apawa (Yn 19:33-34,38; Mt 27:58).

W. Basi tabiri uwaambie, Bwana Mungu asema hivi: Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Waisraeli. Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu na kuwatoa katika makaburi, enyi watu wangu, nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza asema Bwana. (Eze 37:12-14).

Tuombe: Ee Yesu, ulimrudishia Baba yako wa mbinguni kila alichokupa. Nasi ukatupa kila kitu ulichokuwa nacho, hadi ukatoa uzima wako kwa ajili yetu. Kwa fumbo la sakramenti ya ubatizo na Ekaristi umetufanya wana wa Mungu. Kwa nguvu ya sakramenti hizi tujalie tuweze kujitoa kabisa kwa ajili ya kazi ya kueneza ufalme wa Mungu hapa duniani tukifuata mfano wako wa kujitoa kabisa. Amina.

KITUO CHA KUMI NA NNE - YESU ANAZIKWA KABURINI
P: Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani, akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akaviringisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. Wale wanawake walioandamana na Yesu toka Galilaya wakaliona lile Kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa. Halafu walirudi nyumbani kwao, wakawa wanayatayarisha manukato na marashi kwa ajili ya mwili wake (Mt 27:59-60; Lk 23:55-56).

W: Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake: Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua: Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake: Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki. Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu. Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa. Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji (Isa 53:9-12).

Tuombe: Kaburi lako Yesu linaficha ndani yake fumbo la chanzo cha uzima mpya. Kila siku tunatembea kuelekea kaburi letu. Tunaomba uzima uliotoka katika kaburi lako siku ile ya ufufuko uwe mwanga kwetu tunapotembea hapa duniani ili nasi siku ya mwisho tufufukie huo uzima mpya. Amina

SALA YA MWISHO
Yesu wangu, kwa uchungu wote ulioona juu ya msalaba, na kwa kuzimia kwako kwa ukali wa mateso, unijalie nguvu ya kuvumilia kwa moyo taabu zote sasa na saa ya kuzimia kwangu. Nawe Maria Mamangu, kwa uchungu wote ambao moyo wako umejaa ulipomwona Mwanao mpenzi kuinama kichwa na kuzimia, unifadhili nife kifo chema.

(Kutoka “NJIA YA MSALABA INAYAGOMBEA KATIKA BIBLIA” - kimetungwa na Pdr. Thadei A. Mworia, OSS (Tabora, Tanzania)

No comments:

Post a Comment