Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

JUMA LA PILI LA KWARESMA - NJIA YA MSALABA


Sala ya kuanzia Ibada:
Yesu Mkombozi wetu tunakuja mbele yako kutafakari ulivyoteswakwa ajili yetu. Tunaomba tafakari hii itusaidie kupendana zaidi, na kusaidiana kuishi magumu tunayokutana nayo katika maisha yetu. Kwa Sala hii yenye kutafakari juu ya haki na amani, tunakuomba utusaidie tutambue kwamba wewe umekuja kati yetu kushiriki maisha yetu na kutuonyesha njia ya kuepuka dhambi na uovu kwakufuata mafundisho yako.

Ee Yesu mwema, Bikira Maria Mama yako alikuwa nawe katika njia yako ya msalaba. Nasi tunamwomba awe nasi katika sala hii ya Njia ya Msalaba ili hatimaye tunaposhiriki kujenga jamii iliyo bora zaidi, tupate nguvu na msaada kwa njia ya maombezi yake.

Kituo cha Kwanza
YESU ANAHUKUMIWA AFE
Katika jamii yetu tunawakuta watu wengi wanaonyimwa haki zao. Mbinu zinazotumiwa kupotosha haki za watu ni pamoja na ucheleweshaji wa kesi unaoambatana na kupotea kwa majalada kunakoambatana na rushwa. Mfumo mzima unaohusika na utetezi wa haki za watu una kasoro nyingi. Tujifunuo mbele ya Mwonyozi Mungu tuone ni kwa njia zipi tumewakosea watu haki.

Ee Yesu, wewe ulikuja kuwaponya wenye dhambi. Tunakuomba utusamehe kwamakosa yetu ya kupotosha haki, hasa pale tuliposhiriki rushwa au udanganyifu. Tunakuomba utusaidie kuvishinda vishawishi vinavyotuvuta kupotosha haki za watu wako, hasa watu wanyonge na maskini

Kituo cha Pili
YESU ANAPOKEA MSALABA
Tukichunguza jamii yetu tunaona watu mbalimbali ambao wanatumikia adhabu wasiostahili. Miongoni mwa hawa ni wale waliomo magerezani kwa tuhuma za uongo, ama hukumu zisizo za haki, wanyonge wanaonyanyaswa na kunyimwa haki zao zikiwemo huduma za kijamii na hivyo kuishi maisha duni na ya mateso. Wapo pia wale wanaouawa kwa tuhuma za wizi. Ni mambo ya namna hii ndio tunaitwa kuyatafakari leo na kutambua kuhusika kwetu.

Ee Yesu, tunakuja kwako kukuomba utusaidie kubadilika nakuacha kufanya mambo yanayoleta mateso na shida kwa wengine. Utusaidie mateso tunayoyapata tuyapokeekama changamoto ya kukua kiroho na kiutu. Pia utujalie moyo wa kushiriki mateso yanayowakabili wenzetu na tufanye kazi kwa bidii katika kupunguza shida na mateso miongoni mwetu.

Kituo cha Tatu
YESU ANAANGUKA MARA YA KWANZA
Umaskini ni mzigo unaoielemea jamii yetu na kutuangusha wengi dhambini. Vijijini na mijini hali ya maisha ya wanyonge ni mbaya. Mahitaji na huduma muhimu ni mambo magumu kwa wanyonge kuyafanikisha - hata wengine hufa kwa kukosa tiba. Hali ya umaskini inachangiwa kwa kiasi kikubwa na sera pamoja na mipango mibovu na tabia ya kutowajibika. Uvivu, rushwa na ufisadi, ubinafsi, uchoyo, matumizi mabaya ya muda na mali, yote haya hukwamisha jitihada zinazofanywa dhidi ya umaskini.Tumwombe Mungu atusaidie kuwa na moyo wa uwajibikaji na kusaidiana, na hasa kujali manufa na maslahi ya kila mmoja.

Ee Yesu, Mfalme wa Haki naAmani uwajalie maskini wote moyo wa kuungana na kuwajibika katika kukabiliana na umaskini kwa kufanya kazi kwa bidii na kushauri marekebisho ya sera na mipango mibovu. Uwaangazie wanaojinufaisha kutokana na umaskini wa wanyonge watambue ubaya wake, utusaidie kuushinda ubinafsi na uchoyo miongoni mwetu, tukatimize agizo lako la kufanya kazi ya kuleta nafuu ya maisha ya watu wako.

Kituo cha Nne
YESU ANAKUTANA NA MAMA YAKE
Kwenye jamii zetu tunakutana na watu wanaoteseka kwa shida, dhiki na mateso ya aina mbalimbali. Watu hawa wanaweza kuwa familia zinazofarakana na kukosa amani, yatima na wajane, wagonjwa, wanyonge na wahitajimbalimbali. Pia wapowatu miongoni mwetuwanaotawaliwa na pesa, mali na madaraka na kuusahau ukweli. Watu wa aina hii tunakutana nao kila wakati. Tujiulize na kutafakari kama katika hali hiyo tunasaidianaje? Pia kila mmoja wetu ajiulize anawasaidia namna gani watu wenye shida ndani ya familia na katika jumuiya yake.

Ee Yesu, wewe ulikuja ili tuwe na uzima tena tuwe nao tele, (rejea Yn 10: 10). Tunakusihi utusaidie tushirikiane na kutumia vipaji vyetu katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mengi ndani ya jamii yetu ambayo yanawaletea watu wako mateso na kuwakosesha amani. Tunaomba kwa maombezi ya Mama yako tukubali kutumika kama vyombo vyako vya kujenga amani.

Kituo cha Tano
SIMONI WA KIRENE ANAMSAIDIA YESU
Katika maisha yetu tunakutana na watu walio taabani kwa mateso. Hawa wanahitaji msaada wa wengine na zaidi ya yote wanahitaji kumwendea Yesu aliyesema “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mt 11: 28). Nasi tunaalikwa kusaidia watu katika kubeba Msalaba wao unaowaelemea kwa njia ya sala, uwajibikaji na kujali manufaa ya wote na pia kujitolea kwa ajili ya wengine.

Ee Yesu tunakuomba utusaidie tuwe na bidii na ushupavu wa kusaidiana katika shida na mateso ya watu miongoni mwetu. Utuimarishe tudumu katika sala na kushiriki mateso na shida za wengine, ili tuweze kuenenda pamoja nawe katika safari yetu ya pamoja hapa duniani.

Kituo cha Sita
VERONIKA ANAPANGUSA USO WA YESU
Katika kituo hiki tutafakari jinsi wengi tunavyobaki kuangalia tu uovu ukiendelea kutendeka bila kuchukua hatua, na kwa kufanya hivyo tunaufanya uovu uwe ni kitu cha kawaida katika jamii yetu. Tutafakari hali ya huduma katika shule zetu na katika zahanati na hospitali zetu. Huduma kwa jumla ni duni kwa walio wengi wakiwemo wale wanaokosa ndugu wa kuwasaidia. Hapa tunapokea wito wa pekee kama anavyotufundisha na Veronika, tukijua kwamba hizi ni huduma muhimu kwa kila mwanadamu, na ni haki kwa ki la mmoja.

Ee Yesu, Mfalme wa Haki na Amani, tunakuomba utujalie ushujaa na ujasiri wa Mtakatifu Veronika. Katika maisha yetu ya kila siku, tuweze bila woga kuheshimu, kulinda na kutetea haki za watu hasa katika huduma ya elimu na afya. Tunakuomba utujalie umoja na mshikamano kwa kuwa ndio njia bora itakayotusaidia kutimiza wito huo kikamilifu.

Kituo cha Saba
YESU ANAANGUKA MARA YA PILI
Katika jamii yetu tunakutana na watu wengi walio katika shida na mateso makubwa kama ukosefu wa maji safi na salama, ukosefu wa mahitaji muhimu, uduni wa huduma mbalimbali, hali mbaya ya Magereza, na mazingira machafu. Kwa baadhi yetu hali ni taabani na watu wamefika hatua ya kukata tamaa. Njia ya kuwasaidia walio taabani ni kutoa misaada, kurekebisha sera na mipango mibovu na kusukuma utekelezaji wa mipango na sheria nzuri. Pia yatupasa kuchukua wajibu wetu wa pamoja kama jamii katika kuboresha maisha yetu. Yatupasa tujue kwamba njia ya ukombozi wetu ni kubeba msalaba kama Yesu mwenyewe. Tunapokutana na magumu tusikate tamaa kwani Mungu yuko nasi na ndiye tumaini letu.

Ee Yesu, wewe umetufundisha kuwa tutapata tuzo kwa kuwasaidia na kuwahudumia wenye shida mbalimbali, (rej. Mt 25:40,45). Utusaidietufanyebidii kuondoa shidazinazowakabili watu wako.

Kituo cha Nane
WANAWAKE WANAMLILIA YESU
Tunapotafakari kituo hiki, tunajifunza kuwa na moyo wa huruma, kwa Yesu mteseka katika watu wenye shida na mateso mbalimbali. Hawa ni pamoja na wajane na yatima wanaodhulumiwa haki yao ya urithi, wanawake wanaonyanyasika katika familia zao, walezi wanaolemewa mzigo wa kutunza na kulea yatima.

Ee Yesu, unatuambia "Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema” (Mt 5: 7). Tunakuomba utusaidie moyo wa huruma na kutuwezesha kuionyesha huruma yetu kimatendo kwa wote tunaokutana nao kila siku ya maisha yetu.

Kituo cha Tisa
YESU ANAANGUKA MARA YA TATU
Sisi leo, tumwone na kumtafakari Yesu anayelemewa na msalaba na mateso na kuanguka mara ya tatu katika waathirika wa ukimwi. Hawa ni watu wenye mateso makali kimwili, kifikra na hata kiroho. Ni watu ambao tayari jamii imekwishawahukumu. Pamoja na majeraha yake, Yesu anainuka na kuendelea na safari ya ukombozi. Yesu anatualika nasi tusibaki katika huzuni na kukata tamaa bali tuinuke na kuendelea kwani naye anateseka katika mateso yetu, na ndiye tumaini letu. Tuwakumbuke hawa kwa moyo wa huruma na ukarimu, tukijua kwamba Mungu ni mwema na mwenye huruma kwetu sote. Pamoja na waathirika tuwaangalie yatima na wajane wa janga la ukimwi. Tuwasaidie pia walezi ambao wanabeba wajibu wa kuwalea na kuwatunza yatima wakati wao wenyewe hawana uwezo. Sisi sote tujitafakari na tufanye bidii kujiheshimu na kuepuka vitendo vinavyoendeleza maambukizi ya ukimwi.

Ee Yesu, tunakushukuru kwa kuwa Ukombozi wako ni kwa ajili yetu sote. Tunawaombea waathirika wote wajue kwamba mateso yao sio mwisho wa yote. Tunaomba msaada wako ili tuweze kuishi nao vizuri na kuwasaidia. Tupe uchaji wa kutambua ubaya wa dhambi ya uzinzi na uasherati ili kuepukana na janga hilo. Na tunakusihi utujalie ufahamu wa kupata tiba ya ugonjwa huo.

Kituo cha Kumi
YESU ANAVULIWA NGUO
Tunapotafakari moja ya hitaji muhimu kwa mwanadamu ambalo ni mavazi tunaona kuna kasoro nyingi. Miongoni mwetu wapo watu wengi ambao hawawezi kujipatia mavazi kwa ajili ya kusetiri mwili, wengine wananunua mavazi mengi na ya fahari kama kufuru mbele ya Mungu. Baadhi wanavaa mavazi yanayoonyesha kutoheshimu utu wao.Tunaitwa leo kujitafakari kibinafsi na kama jamii kuona upotevu huo na kurekebisha.

Ee Yesu, tunakuomba utufungue macho ya mioyo yetu tupate kuuona ubaya wetu katika matumizi ya mavazi, na kujua kwamba mavazi ni hitaji msingi kwa kila mwanadamu. Tunakuomba utuwezeshe kujirekebisha na kuwa na moyo wa ukarimu kwa wanaokosa mavazi na pia kushiriki katika kupunguza umaskini ili kila mmoja aweze kujipatia mahitaji msingi.

Kituo cha Kumi na Moja
YESU ANASULUBISHWA MSALABANI
Hapa Yesu ni kielelezo cha watu wanaoteseka. Nasi twaweza kuwa tumechangia katika kuleta mateso kwawengine. Miongoni mwetu wako walioingia katika mateso kwa sababu ya kutetea na kuwasaidia walio katika matatizo na shida mbalimbali. Baadhi yetu tumeshiriki vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, na wengine tumeiba fedha, mali na rasilimali ya umma hata kuingia katika ufisadi, na kwa njia hii kusababisha maisha duni kwa wenzetu. Hali mbaya ya maisha ya watu imeleta hasira ya jamii ambayo inaendelea kuenea katika nchi yetu. Vitendo vinavyodhihirisha hasira ya jamii ni vingi, na matokeo yake natari kwa jamii yetu na taifa letu.Yesu anatufundisha kujitoa sadaka na kutuonya tuepuke mambo yanayosababisha mateso kwa watu wake. Pia anatuonya kuepuka kuwaka hasira kwani itaangamiza jamii yetu. Badala yake anatualika tushiriki sote kuhakikisha maisha bora kwa wote, na hivyo amani yetu iweze kudumu.

Ee Yesu, tunakuomba utujalie moyo wa ujasiri katika kutetea haki na kuwasaidia walio katika mateso. Utusaidie kuepuka vitendo vinavyowaletea watu wako mateso. Tunaomba neema na msaada wako katika kukamilisha nia ya kujenga ushirikiano kati yetu na kujali manufaa na maslahi ya wote.

Kituo cha Kumi na Mbili
YESU ANAKUFA MSALABANI
Tumwangalie Yesu anayekufa msalabani bila hatia, akibeba dhambi zetu ili tupate kuokoka. Nasi tuna wajibu wakushiriki kazi ya ukombozi wa mwanadamu kimwili na kiroho. Wajibu huo ni katika familia zetu, jumuiya, taifa na jamii nzima. Tukitimiza vizuri wajibu zetu, tunaendeleza kazi ya ukombozi. Na mwisho wa yote tutaweza nasi kusema pamoja na Yesu, “yametimia.”  Kama binadamu tunashindwa mara kadhaa kwa sababu ya udhaifu wetu hata kusababisha vifo bila sababu miongoni mwetu. Tumwombe toba Yesu pale tuliposhindwa, na tunapomtafakari Yesu aliyekufa msalabani, tumpe nafasi afishe ndani mwetu na kati yetu udhaifu wetu na kasoro zinazokwamisha kazi ya ukombozi wa mwanadamu.

Ee Yesu, uliyekufa Msalabani kwa ajili ya Ukombozi wetu, tunakuomba utusaidie tushiriki kikamilifu kazi ya ukombozi na ufishe ndani mwetu na katika mifumo na miundo yetu udhaifu unaokwamisha kazi ya ukombozi katika jamii yetu.

Kituo cha Kumi na Tatu
YESU ANASHUSHWA MSALABANI
Yesu anashushwa msalabani akiwa amekamilisha kazi yake, yaani mpango wa Mungu wa ukombozi wetu. Kwa maisha yetu sote zawadi ya uhai ina lengo. Tumekuja duniani tukiwa pia tumepewa wajibu. Ndio kuboresha maisha yetu, ya jamii na mazingira tunamoishi kwa faida ya kizazi cha sasa na vile vijavyo. Tumekwishaona maeneo mengi ya uwajibikaji wetu kwakadiri ya mafundisho ya Maandiko na hali tunamoishi leo. Tunapoendelea na safari yetu ya kushiriki ukombozi, tutumie nafisi na vipaji vyetu kikamilifu kutimiza mafundisho ya Neno katika maisha yetu ya kila siku.

Ee Yesu, tunataka kuweka ahadi leo ya kukufuata kwa matendo, mienendo na fikra zetu. Kuweza kutimiza ahadi yetu tunahitaji msaada wako. Ee Yesu uwe nasi.

Kituo cha Kumi na Nne
YESU ANAZIKWA KABURINI
Ndani yako Yesu, tunataka kuzika udhaifu wetu wa kibinafsi na wa kijamii. Sisi tunapo kutafakari katika njia yako ya Msalaba tunatambua wajibu wetu wa kujitoa sadaka. Tuna mengi uliyotujalia, lakini tunavutwa kuyatumia vibaya ama kutoyatumia kabisa. Tunataka kuzika yote yanayotukwamisha na tunakuomba utusaidie tudumu katika uwajibikaji Kikristu.

Ee Yesu tunatamani sana kutekeleza nia zetu, lakini tunajua tunahitaji msaada wako. Tunakuomba tunapofanya bidii kutekeleza nia hizo wewe uwe nasi kila wakati.

SALA YA MWISHO

Ee Yesu, tunaomba tafakari tuliyofanya na sala tuliyoisali itusaidie kuwa wakamilifu ili tuweze kuyashinda maovu. Utupe ujasiri wa kutetea ukweli, haki na amani. Kwa kazi yetu, tuweze kuleta faraja kwa wale wenye mateso. Ee Yesu, tunaomba msaada na neema yako ili tuweze kuziweka nia zetu katika matendo yetu ya kila siku. Tunaomba Bikira Maria Mama yako awe nasi katika maisha yetu. Maombi yake yatusaidie tuwe na moyo wa kujitakatifuza na kujenga jamii yenye misingi ya Ukweli, Haki na Amani.

Kabla ya kila kituo: 
K: Ee Yesu tunakuabudu, tunakushukuru;
W: Kwa kuwa umewakomboa watu kwa msalaba wako mtakatifu.


Baada ya kila kituo:
'Baba Yetu, 'Salamu Maria' na 'Atukuzwe Baba',


K: Ee Bwana utuhurumie! W: Utuhurumie!
K: Roho za waamini marehemu, wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa amani. W: Amina


(Kutoka “NJIA YA MSALABA KATIKA TAFAKARI YA HAKI NA AMANI” - Kitabu kimechapishwa Tume ya Haki na Amani - TEC, Dar es Salaam (Aprili 2004))

No comments:

Post a Comment