Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, FEBRUARI 21, 2023



MASOMO YA MISA, FEBRUARI 21, 2023
JUMANNE, JUMA LA 7 LA MWAKA


SOMO 1
YbS. 2:1 – 11

Mwanangu, ukija kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kwa kujaribiwa. Ujitengeneze moyo ustahimili, wala usitaharuki siku ya kuteswa. Uambatane naye wala usijitenge tena, ili mwisho wako ukuzwe. Kila utakalopelekewa ulipokee kwa kuchangamka moyo, uyavumilie mabadiliko ya unyonge wako. Maana dhahabu hujaribiwa moto na watu wateule kalibuni mwa unyonge. Basi, umwamini Yeye, naye atakusaidia; ukazinyoshe njia zako, na kulikaza taraja lako katika Yeye.

Enyi mnaomcha Bwana, Zingojeeni upande msije mkaanguka. Enyi mnaomcha Bwana, Mwaminini Yeye sana, Thawabu yenu haitawapotea. Enyi mnaomcha Bwana, Sasa tarajieni mema, na furaha ya daima na rehema.

Angalieni vizazi vya kale mkaone; Nani aliyemtumaini Bwana akaaibika? Nani aliyekaa hali ya kumcha akaachwa? Nani aliyemwita akadharauliwa? Mradi Bwana yu mwenye huruma na rehema, Husamehe dhambi na kuokoa wakati wa shida.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 37:3 – 4, 18 – 19, 27 – 28, 39 – 40 (K) 5

(K) Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.

Umtumaini Bwana ukatende mema, 
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako. (K)

Bwana anazijua siku za wakamilifu,
Na urithi wao utakuwa wa milele.
Hawataaibika wakati wa ubaya,
Na siku za njaa watashiba. (K)

Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
Wala hawaachi watauwa wake. (K)

Na wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa. (K)



SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, ee Bwana, ni ambayo yamethibitika milele na milele.
Aleluya.



INJILI
Mk. 9: 30 – 37

Yesu na wanafunzi wake wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza.

Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea motto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment