MASOMO YA MISA, FEBRUARI 8, 2023
JUMATANO, JUMA LA 5 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. BAKHITA
SOMO 1
Mwa. 2:4 – 9, 15 – 17
Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi
hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa
maana Bwana Mungu hajainyesha nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;
ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. Bwana Mungu
akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi,
akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.
Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki
wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu akachipusha
katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa
uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Bwana Mungu
akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Bwana
Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku
utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 104:1 – 2, 27 – 30 (K) 1
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Umejivika heshima na adhama.
Umejivika nuru kama vazi;
Umezitandika mbingu kama pazia; (K)
Hao wote wanakungoja Wewe,
Uwape chakula chao kwa wakati wake.
Wewe huwapa,
Wao wanakiokota;
Wewe waukunjua mkono wako,
Wao wanashiba mema; (K)
Wewe wauficha uso wako,
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wan chi. (K)
SHANGILIO
Zab. 19:8
Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.
INJILI
Mk. 7:14 – 23
Yesu aliwaita makutano tena, akawaambia,
NIsikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia
chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule
mtu. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.
Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano,
wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi
hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia,
hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha
chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema,
Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu
hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi,
hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu
yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment