MASOMO YA MISA, FEBRUARI 7, 2023
JUMANNE, JUMA LA 5 LA MWAKA
Mwa. 1:20 – 2:4
Mungu alisema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu
kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. Mungu
akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji
yalijawa navyo kwa wingi kw ajinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake;
Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke,
mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. Ikawa jioni ikawa
asubuhi, siku ya tano.
Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi
zake, mnyama wa kufungwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi
zake; ikawa hivyo. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa
kufungwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitaambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake;
Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu;
kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama,
na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu
akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba.
Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni,
mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na
ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu
akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wan chi yote,
pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu;
na chakula cha kila mnyama wan chi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila
kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula
chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema
sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.
Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake
lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe
siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia
siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha
kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.
Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi
zilipoumbwa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 8:3 – 8 (K) 1
(K) Wewe Mungu, Bwana wetu,
jinsi lilivyo tukufu
jina lako duniani mwote.
Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie? (K)
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
Kondoo, na ng’ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni;
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za baharini. (K)
SHANGILIO
Zab. 27:11
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuniongoza
katika njia iliyonyoka.
Aleluya.
INJILI
Mk. 7:1-13
Mafarisayo, na badhi ya waandishi waliotoka
Yerusalemu, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakaona wengine katika wanafunzi wake
wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na
Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya
wazee wao; tena wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine
waliyopokea kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba.
Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza,
Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula
kwa mikono najisi? Akawambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki,
kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali
nami; Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu.
Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika
mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema? Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika
mapokeo yenu. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na,
amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia
babaye au mamaye. Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu chochote kikupasacho
kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye
au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena
mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment