MASOMO YA MISA, FEBRUARI 6, 2023
JUMATATU, JUMA LA 5 LA MWAKA WA KANISA
KUMBUKUMBU YA MT. PAULO MIKI NA WENZAKE
SOMO 1
Mwa. 1:1 – 19
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo
nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya
maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.
Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu
akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mugu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru
mchana, na giza akliita usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja.
Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji,
likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo
juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile
anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi siku ya pili.
Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na
yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita
pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa
ni vyema.
Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao
mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo
ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa
jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi
yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.
Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la
mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na
siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya
nchi; ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale
mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka
katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku na
kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi,
siku ya nne.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 104:1 – 2, 5 – 6, 10, 12, 24, 35 (K) 31
(K) Bwana na ayafurahie matendo yake.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu, umejifanya mkuu sana.
Umejivika heshima na adhama,
Umejivika nuru kama vazi. (K)
Uliiweka juu ya misingi yake,
Isitikisike milele,
Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi,
Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. (K)
Hupeleka chemchemi katika mabonde;
Zapita kati ya milima,
Kando kando hukaa ndege wa angani,
Kati ya matawi hutoa sauti zao. (K)
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Kwa hekima umevifanya vyote pia,
Dunia imejaa mali zako.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. (K)
SHANGILIO
Zab. 111:7, 8
Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, ee Bwana, ni amini,
yamethibitika milele na milele.
Aleluya.
INJILI
Mt. 6:53-56
Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka
walifika nchi ya Genezareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara
watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua
vitandani walio hawawezi kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila
alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa
sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment