MASOMO YA MISA, FEBRUARI 5, 2023
DOMINIKA YA 5 YA MWAKA A WA KANISA
MWANZO:
Zab. 95:6 – 7
Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za
Bwana aliyetuumba; kwa maana ndiye Mungu wetu.
SOMO 1
Isa. 58:7 – 10
Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na
kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike
nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako
itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako
itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na
Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo
kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu
mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako
itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 112:4 – 9 (K) 4
(K) Nuru huwazukia wenye adili gizani.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki. (K)
Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele.
Hataogopa habari mbaya;
Moyo wake u imara ukimtumaini Bwana. (K)
Moyo wake umethibitika hataogopa,
Hata awaone watesi wake wameshindwa.
Amekirimu na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu. (K)
SOMO 2
1Kor. 2:1 – 5
Ndugu zangu, mimi nilipopkuja kwenu, sikuja
niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana
naliazimu nisijue neno lolote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa. Nami
nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno
langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili
za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili Imani yenu isiwe katika
hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Mdo. 16:14
Aleluya, aleluya,
Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza
rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo
wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:13 – 16
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ninyi ni chumvi ya
dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena
kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji
hauwezi kusitirika ukiwa juu yam lima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini
ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo
hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema,
wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment