MASOMO YA MISA, FEBRUARI 2, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 4 LA MWAKA
SIKUKUU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI
SOMO 1
Mal. 3:1-4
Bwana Mungu asema hivi: Angalieni, namtuma
mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta
atalijilia hekalu lake ghafula; naam yule mjumbe wa agano mnayemfurahia,
angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili
siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana
yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye
nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa
Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika
haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za
Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
ZAB. 24:7-10 (K) 8
(K) Ni nani Mfalme wa utukufu? Ni Bwana.
Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inukeni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K)
Ni nani Mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu, hodari,
Bwana hodari wa vita. (K)
Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele
Mfalme wa utukufu apate kuingia. (K)
Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Bwana wa majeshi,
Yeye ndiye Mfalme wa utukufu. (K)
SOMO 2
Ebr. 2:14-18
Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili,
yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye
aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba
maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni
hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo
ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu
mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za
watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao
wanaojaribiwa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Lk. 2:32
Aleluya, aleluya!
Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa
utukufu wa watu wako Israeli.
Aleluya!
INJILI
Lk. 2:22-40
Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo
torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa
Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye
kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama
ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Huwa wawili au makinda ya njiwa wawili. Na
tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye
haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu
yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya
kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi
walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,
yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,
Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani,
kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari
machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa, na kuwa utukufu wa watu
wako Israeli.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment