Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, FEBRUARI 16, 2023


MASOMO YA MISA, FEBRUARI 16, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 6 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Mwa. 9:1 – 13

Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi. Kila mnyama nwa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani; pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyoawapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote. Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu.

Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na wanadamu; maana kwa mkono wake Mungu alimfanya mwanadamu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake.

Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichopo pamoja nayi, ndege, kila mnyama wa kufugwa, na kil amnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo kuiharibu nchi.

Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kil akiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 102:15 – 20, 28, 21 – 22 (K) 19

(K) Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi.

Mataifa wataliogopa jina la Bwana.
Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Atakapoonekana katika utukufu wake,
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao. (K)

Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
Na watu watakaoubwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)

Wana wa watumishi wako watakaa,
Na wazao wataimarishwa mbele zako.
Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
Na sifa zake katika Yerusalemu.
Pindi mataifa watakapokusanyika pamoja,
Falme nazo ili kumtumikia Bwana. (K)



SHANGILIO
Zab. 147:12, 15

Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.



INJILI
Mk. 8:27 – 33

Siku ile Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, WAtu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohane Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake.

Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

Neno la Bwana… Sifa kwa ko Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment