MASOMO YA MISA, FEBRUARI 15, 2023
JUMATANO, JUMA LA 6 LA MWAKA
SOMO 1
Mwa. 8:6 – 13, 20 – 22
Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua
dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na
huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji
yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa
mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi
yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na
siku saba tena, akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni,
na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda,
basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba
tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe.
Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa
kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa
kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka.
Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akamtwaa katiak
kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za
kuteketezwa juu ya madhabahu. Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana
akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu,
maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga
tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda nchi idumupo,
majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa
kaskazini na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 116:12 – 15, 18 – 19 (K) 17
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru , ee Bwana.
Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu,
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake. (K)
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote,
Katika nyua za nyumba ya Bwana,
Ndani yako, ee Yerusalemu. (K)
SHANGILIO
Efe. 1:19 – 27
Aleluya, aleluya,
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo ayatie nuru macho
ya mioyo yetu, tujue tumaini la mwito wetu jinsi lilivyo.
Aleluya.
INJILI
Mk. 8:22 – 26
Siku ile, Yesu na wanafunzi wake, wakafika
Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. Akamshika mkono yule kipofu,
akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake,
akamwuliza, Waona kitu? Akatazama juu, akisema, Naona watu kama miti,
inakwenda. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama
sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. Akampeleka nyumbani kwake akisema,
Hata kijijini usiingie.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment