MASOMO YA MISA, FEBRUARI 13, 2023
JUMANNE, JUMA LA 6 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Mwa. 4:1 – 15, 25
Adamu alimjua Hawa mkewe; naye akapata mimba,
akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana. Akaongeza akamzaa
ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima
ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili
naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama.
Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumakabali, wala sadaka
yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Bwana akamwambia Kaini,
Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema,
hutapata kibali? Usipotenda vyma dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo
inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye,
twende uwandani. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,
akamwua.
Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu
yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini?
Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa
wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono
wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoto na mtu asiye na
kikao duniani. Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa,
haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali
na uso wako, nami niakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa
kila anionaye ataniua. Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo yeyote atakayemwua
Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye
asije akampiga.
Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana
mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao
mwingine mahali pia Habili; kwa sababu Kaini alimwua.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:1, 8, 16 – 17, 20 – 21 (K) 14
(K) Umtolee Mungu dhabihu za kushukuru.
Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima. (K)
Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia,
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
Umekaa na kumsengenya ndugu yako,
Na mwana wa mama yako umemsingizia.
Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Walakini nitakukemea;
Nitayapanga hayo mbele ya macho yako. (K)
SHANGILIO
1Sam. 3:9
Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia:
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
INJILI
Mk. 8:11 – 13
Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na
Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni
mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni,
Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake
hata ng’ambo.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment