MASOMO YA MISA, FEBRUARI 11, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 5 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Mwa. 3:9 – 24
Bwana Mungu alimwita Adamu, akamwambia, Uko
wapi? Akasema, nalisikia sauti yako bustanini, naliogopa kwa kuwa mimi ni uchi;
nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe
matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa
awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. Bwana Mungu
akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka
alinidanganya, nikala.
Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu
umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote
walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha
yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na
uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia
uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa
kwa mumeo, naye atakutawala.
Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya
mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi
imelaani kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha
yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho
la uso wako utakula chakula , hata utakapoirudia ardhi, ambayo kaitka hiyo
ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.
Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa
yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai. Bwana Mungu akawafanyia Adamu na
mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa
kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake
akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu
akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.
Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya
Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 90:2 – 6, 12 – 13 (K) 1
(K) Wewe Bwana, umekuwa makao yetu, kizazi baada
ya kizazi.
Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia
Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu. (K)
Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku. (K)
Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka. (K)
Utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uhurumie watumishi wako. (K)
SHANGILIO
Zab. 25:4, 5
Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe
mapito yako.
Aleluya.
INJILI
Mk. 8:1 – 10
Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena
ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, Yesu aliwaita wanafunzi wake,
akawaambia, Nawahurumia mkutano kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala
hawana kitu cha kula; nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga,
watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali. Wanafunzi wake wakamjibu, Je!
Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani? Akawauliza, Mnayo
mikate mingapi? Wakasema, Saba.
Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile
mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake waaandikie;
wakawaaandikia mkutano. Walikuwa na visamaki vichache; akavibariki, akasema
wawaandikie na hivyo pia. Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya
mikate makanda saba. Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga. Mara akapanda
chomboni pamoja na wanafunzi wake, akaenda pande za Dalmanutha.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment