MASOMO YA MISA, FEBRUARI 10, 2023
IJUMAA , JUMA LA 5 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. SKOLASTIKA, BIKIRA
SOMO 1
Mwa. 3:1 – 8
Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa
mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema
Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka,
Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati
ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia
mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula
matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema
na mabaya.
Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa
chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa
katika matunda yake akala, akampa na mumewe, anaye akala. Wakafumbuliwa macho
wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia
nguo.
Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea
bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya
bustani, Bwana Mungu asiwaone.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 32:1 -2, 5 – 7 (K) 1
(K) Heri aliyesamehewa dhambi.
Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila. (K)
Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. (K)
Kwa hiyo kila mtu mtauwa
Akuombe wakati unapopatikana.
Hakika maji makuu yafurikapo,
Hayatamfikia yeye.
Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
Utanizungusha nyimbo za wokovu. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:34
Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.
INJILI
Mk. 7:31 – 37
Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita
katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya
Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono.
Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema
mate, akamgusa ulimi, akataama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana
yake, Funguka mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea,
akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi
kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi,
wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment