Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

HAKI YA MUNGU INAKAMILISHWA NA HURUMA


“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila jumapili
Jumapili, Februari 19, 2023
Dominika ya 7 ya Mwaka A wa Kanisa

Law 19: 1-2,17-18;
Zab 102: 1-4, 8, 10, 12-13;
1 Kor 3: 16-23;
Mt 5:38-48.


HAKI YA MUNGU INAKAMILISHWA NA HURUMA


Katika jamii za zamani ambazo zilikuwa hazikuwa na nguvu ya Nchi yakuweza kuweka taratibu na sheria, watu walikuwa wakilipana kisasi kwa urahisi tu bila hata ya kuwa na kikomo. Aliyefanya kosa nakutambulika alikuwa akipewa adhabu ambayo ni mfano kwa wengine, adhabu kali ya hadharani ambayo kila atakaye ona hata thubutu kufanya kosa kama hilo. Kisasi ilikuwa ni aina ya kulipiza, lakini ilikuwa ni kitendo cha kinyama cha kutenda haki. Ilikuwa ni kukomesha hali kama hizi ndio maana Torati iliwekwa kwamba “jino kwa jino, jicho kwa jicho” (Kutoka 21:23-25). Hii ndio sheria ilio tafsiriwa vibaya katika historia. Kila mmoja alikuwa amlipe mtu kadiri au sawa sawa na kola alilotendewa, na sio zaidi. Kama ilifanyika hivyo, inaonekana kuhukumu sawa kwa haki. Lakini Yesu hapendezwi nayo wala haoni ni sawa. Anaelekeza kwenda juu zaidi badala ya kuwa na hii sheria kali, na anaelekeza kukabili tatizo katika hali tofauti.

Marabi wa kipindi cha Yesu walifundisha. “Uwawa, lakini usiue” na kuongeza mara kwamba ; kama mtu akikuvamia na anataka kuchukua maisha yako, usifikiri, usijisemee mwenyewe kwamba kama nikimuuwa huyu damu yake itakuwa juu yangu; muuwe kwanza kabla hajakuuwa! Maelekezo haya ya Marabii hayaleti upingamizi wowote. Yanaendana na akili ya kawaida na yalipata pia kuungwa mkono na sheria yenyewe (Tora). Lakini Yesu hakubaliani na hii na anasema kwa wafuasi wake “haupaswi kulipa baya kwa baya! Badala ya kulipa baya kwa ndugu yako, unapaswa uwe tayari kuteseka au kudhulumiwa” (Mt 5:39). Anaongeza kwa kutoa mifano minne alioitoa katika maisha ya kila siku ya watu.

Wa kwanza unaoendana na mashambulizi ya mwili: “mtu akikupiga shavu la kulia”. Yesu anaongelea kuhusu haki kwasababu msukumo wake ni mkubwa. Ni juu ya kupiga, kosa ambalo ni kubwa sana, ambalo lilikuwa kwa kufanya hivyo unalipishwa adhabu ya mshahara wa mwezi mzima na zaidi katika Israeli. Yesu hawaambii wafuasi wawe watu wakwenda kutaka kupigwa. Anawataka wawe na tabia tofauti kabisa, “mpatie na shavu la upande mwingine.” Ni wazi kwamba maneno ya Yesu hayapaswi kuchukuliwa tu kama yalivyo hapo. Yesu mwenyewe alivyopigwa kofi, hakuwapatia upande mwingine, bali aliuliza kwanini wanipiga? (Yn 18:23). Anachotaka kutoka kwa wafuasi anataka wawe na mwamko wa ndani wakukubali kudhulumiwa, kudhalilishwa, badala ya kulipiza kisasi na kuleta maangamizi kwa ndugu zao. Njia pekee ya kuvunja ubaya na mzunguko wake ni kusamehe. Kama mtu akilipiza ubaya kwa ubaya zaidi, ubaya hauondoi ule ubaya wa mwanzo bali unaongeza ubaya zaidi. Mzunguko huu wa ubaya unaweza tu, kuondolewa kwa msamaha wa kweli kutoka ndani.

Mfano wa pili ni juu ya haki za kiuchumi. Katika Israeli, wanaume na wanawake walivaa mavazi mawili: kanzu refu kuanzia shingoni hadi miguuni, ikiwa na mikono mifupi au mirefu, pia skafu. Skafu ilifumuliwa na kufungwa mwilini wakati wa baridi na ilitolewa wakati wa kufanya kazi. Pi ilitumika kama blanketi wakati wa usiku lakini hasa kwa wale maskini. Ndio hii, Torati inayosema isichukuliwe (Kuto 22:25-26). Yesu anatoa mfano huo wa hali ya juu kabisa kuhusu kukosa haki: kama mfuasi ameletwa mahakamani na nguo yake imesha chukuliwa afanyeje? Wakati yote yamesha chukuliwa? Afanye nini? Kwa hili anapaswa kutoa hata ile aliobaki nayo ili isije ikawa kisingizio. Awe tayari kubaki mtupu, kama Bwana wake akiwa juu ya Msalaba

Mfano wa tatu ni kuhusu nguvu/mamlaka. Ilikuwa ikitokea kwamba askari wa Kirumi walikuwa wakiwa nyanyasa maskini kwa kuwaongoza kwa nguvu na kuwalazimisha kubeba mizigo mizito. Mfano, Simoni wa Kirene alilazimishwa kubeba msalaba wa Yesu. (Mt 27:31). Huyu ambae alikuwa Zelote, wana mapinduzi wa wakati huo walishawishi kugoma na kulipiza kisasi kupinga kitendo kama hicho. Yesu anawaambia wafuasi wake “sio sheria ya hekima” tabia hiyo haiwezi kuleta matunda mazuri. Ana waambia wafuasi hata bila ya kukunja moyo wafanye kwa uhuru kabisa bila kupinga kujiepusha na kitendo chochote ambacho sio cha upendo.

Mfano wa nne ni wa yule mtu anayekuja kusumbua kuomba msaada.Yesu anawaambia Wafuasi wake: “wape wanapokuja kukuomba, usimpe mtu kisogo anayetaka msaada wako” (Mt 5: 42). Kama waweza kuafnya kitu fanya.

Yesu mwenyewe alikuja na kuonyesha mfano wa kwenda kinyume na ‘jino kwa jino’ katika hali ya juu. Maisha ya Yesu pale msalaba yanaonesha kwenda sambamba kabisa kwa somo la Injili ya leo, yeye walimpiga makofi lakini hakurudisha, walimchukulia nguo yake hakusema neno, adui zake aliwaombea kwa Baba kwani hawakujua walilokuwa wakilitenda. Yesu pia anawasamehe watesi wake badala ya kulipiza kisasi. Ni sheria ya hali ya juu inayotualika kwenda kwenye haki ya Kimungu. Sheria hii inawezekana tu pale tutakapo ona utakatifu wa Kimungu kwa kila mtu, hata wale tunaodhani ni wadhambi sana. Mungu anatualika tuwapende. Haki ya Mungu inakamilishwa na huruma yake. Kama waweza kuielewa na kuiishi, tutaona mambo makuu yakitokea katika maisha yetu na katika maisha ya wale tulio wasamehe.

Sala: Bwana, nisaidie niweze kusamehe. Nisaidie niweze kuonesha huruma kwa wale walio nidhulumu na kunionea katika maisha yangu. Naomba nisikie maneno yako na kufuata mfano wako ulio onesha pale msalabani uliposali “Baba wasamehe kwani hawajui watendalo”. Nisaidie Bwana niweze kuiga kuishi upendo wako na kuiga maisha yako ya kusamehe. Yesu, nakuamini wewe. Amina

Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment