Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATATU, JANUARI 9, 2023


MASOMO YA MISA, JUMATATU
JANUARI 9, 2023
SIKUKUU YA UBATIZO WA BWANA


SOMO 1
Isa. 42:1 – 4, 6 – 7

Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sharia yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 29:1 – 4, 9 – 10 (K) 11

(K) Bwana atawabariki watu wake kwa Amani.

Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu. (K)

Sauti ya Bwana I juu ya maji
Bwana yu juu ya maji mengi
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina adhama. (K)

Sauti ya Bwana yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake wasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)



SOMO 2
Mdo. 10:34 – 38

Siku ile: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa nay eye.

Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli, akihubiri habari njema ya Amani kwa yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



SHANGILIO
Mk. 9:7

Aleluya, aleluya,
Mbingu zilifunguka na sauti ya Baba ikasikika, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”
Aleluya, aleluya.



INJILI
Mt. 3:13 – 17

Siku ile: Yesu alirudi kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohane ili abatizwe. Lakini Yohane alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.

Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment