Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 5, 2023

MASOMO YA MISA, JANUARI 5, 2023
ALHAMISI YA 2 YA NOELI


SOMO 1
1Yon. 3:11-21

Wapenzi: Hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, nay a ndugu yake yalikuwa ya haki. Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia. Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.

Katika hii tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?

Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendon a kweli. Katika hili tuatfahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tuataituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 100 (K) 1

(K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote.

Mtumikieni Bwana kwa furaha,
Njoni mbele zake kwa kuimba; (K)

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake na kondoo wa malisho yake. (K)

Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake; (K)

Kwa kuwa ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)



SHANGILIO
Ebr. 1:1-2

Aleluya, aleluya,
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi, na kwa namna nyingi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, Siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.



INJILI
Yn. 1:43-51

Siku ile, Yesu alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate. Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro. Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikwa na Musa katiak torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.

Basi Yesu, akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akawaambia, Amin amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment