MASOMO YA MISA, JANUARI 30, 2023
JUMATATU, JUMA LA 4 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Ebr. 11:32 – 40
Ndugu zangu niseme nini tena? Maana wakati
usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi
na Samweli na za manabii; ambao kwa Imani walishinda milki za wafalme,
walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za
moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu,
walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea
wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa,
wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa
dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa
mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga;
walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa
wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa
nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika
mapango na katika mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa
sababu ya Imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia
kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 31:19 – 23 (K) 24
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde,
nyinyi nyote
mnamngojea Bwana.
Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu. (K)
Utawasitiri na fitina za watu
Katika sitara ya kuwapo kwako;
Utawaficha katika hema
Na mashindano ya ndimi. (K)
Bwana ahimidiwe;
Kwa maana amenitendea fadhili za ajabu
Katika mji wenye boma. (K)
Nami nalisema kwa haraka yangu,
Nimekatiliwa mbali na macho yako;
Lakini ulisikia sauti ya dua yangu wakti
nilipokulilia. (K)
Mpendeni Bwana, ninyi nyote mlio watauwa wake.
Bwana huwahifadhi waaminifu,
Humlipa atendaye kiburi malipo tele. (K)
SHANGILIO
Yn. 15:15
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini
ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
INJILI
Mk. 5:1 – 20
Yesu na wanafunzi wake walifika ng’ambo ya
bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana
na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale
makaburini; wal ahakuna mtu yeyote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;
kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile
minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za
kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani,
akipiga kelele na kujikatakatia kwa mawe.
Na laipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio,
akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana
wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe
pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu
ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. Na
hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. Pepo wote
wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa
ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi
lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili;
wakafa baharini.
Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari
mjini na mashamba. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu,
wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, ndiye pepo,
ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi;
wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule
mwenye pepo, na habari za nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao.
Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa
na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda
zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu
aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. Akaenda zake, akaanza kuhubiri
katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment