MASOMO YA MISA
JANUARI 25, 2023
SIKUKUU YA KUONGOKA KWA MT. PAULO, MTUME
SOMO 1
Mdo 22:3-16
Paulo aliwaambia makutano, Mimi ni mtu wa
Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu,
miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi nikawa mtu
wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa njia
hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani wanaume na wanawake. Kama
Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea
barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale
waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia
Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia
pande zote. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona
unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti,
ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami, waliiona ile nuru, lakini
hawakuisikia ile sauti ya Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na
huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni
kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja
nami, nikaingia Dameski.
Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata
sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, akanijia, akasimama
karibu nami akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa
ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake,
na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa
maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na
kuyasikia. Basi sasa unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako,
ukiliitia jina lake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Bwana.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117:1-2 (K) Mk. 16:15
(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri
Injili kwa kila kiumbe.
Aleluya!
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
enyi watu wote, mhimidini. (K)
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 15:16
Aleluya, aleluya,
Niliwachagua ninyi, nikawaweka mwende mkazae
matunda, na matunda yenu yapate kukaa.
Aleluya.
INJILI
Mk. 16:15-18
Yesu alionekana na wale kumi na mmoja,
akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Maana ishara hizi
zintafuatana na hao waaminio, kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha
mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa;
wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Neno la Bwana… Sifa kwako ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment