Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 17, 2023

MASOMO YA MISA, JANUARI 17, 2023
JUMANNE, JUMA LA 2 LA MWAKA WA KANISA

KUMBUKUMBU YA MT. ANTONI (ABATE)

SOMO 1
Ebr. 6:10 – 20

Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmehudumia watakatifu, n ahata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa Imani na uvumilivu.

Kwa maana Mungu, alipompa Ibrahimu ahadi, kwa sababu alikuwa hana mkubwa kuliko yeye mwenyewe wa kumwapa, aliapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika yangu kubariki nitakubariki, na kuongeza nitakuongeza. Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana wairithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu; tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 111:1 – 2, 4 – 5, 9 – 10 (K)

(K) Bwana atalikumbuka agano lake milele.

Aleluya,
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo. (K)

Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
Amewapa wamchao chakula,
Atalikumbuka agano lake milele. (K)

Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele,
Jina lake ni takatifu la kuogopwa,
Sifa zake zakaa milele. (K)



SHANGILIO
Aleluya, aleluya.
Mtu akinipenda atalishika neno langu, na baba yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.



INJILI
Mk. 2:23-28

Ikawa Yesu alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, zamani za kuhani mkuu Abiathari, akaila mikate ile ya Wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila makuhani, akawapa na wenziwe?

Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment