MASOMO YA MISA, JANUARI 12, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 1 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 3:7 – 14
Roho Mtakatifu asema: Leo, kama mtaisikia sauti
yake, msifanye migumu mioyo yenu, kama wakati wa kukasirisha, siku ya
kujaribiwa katika jangwa, hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, wakaona
matendo yangu miaka arobaini. Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, nikasema,
Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; hawakuzijua njia zangu; kama
nilivyoapa kwa hasira yangu, hawataingia rahani mwangu. Angalieni, ndugu zangu,
usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye
hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe
mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama
tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:6 – 11 (K) 8
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu.
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu,
Kama vile huko Meriba, kama siku ya Masa
jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima wakayaona matendo yangu. (K)
Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile,
Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo,
Hawakuzijua njia zangu.
Nikaapa kwa hasira yangu
Wasiingie rahani mwangu. (K)
SHANGILIO
Mt. 11:25
Aleluya, aleluya,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu nan chi, kwa
kuw amambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.
INJILI
Mk. 1:40-45
Siku ile mtu mwenye ukoma akaja kwa Yesu,
akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye
akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na
mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara,
akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa
kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.
Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi,
na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali
alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.
Neno la Bwana… Sifa kwako ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment