MASOMO YA MISA, JANUARI 10, 2023
JUMANNE, JUMA LA 1 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 2:5 – 12
Mungu hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule
ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali Fulani, akisema,
Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?
Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, umemvika taji ya utukufu na heshima,
umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini yake hakusaza
kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa
chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani,
Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili
kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.
Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na
kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu,
kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye
atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni
haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu;
katikati ya kanisa nitakuimbia sifa.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 8:2, 5 – 9 (K) 7
(K) Umemtawaza Mwanao juu ya kazi ya mikono
yako.
Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie? (K)
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako. (K)
Umevitia vitu vyote chiini ya miguu yake,
Kondoo, na ng’ombe wote pia,
Naam, na wanyama wa kondeni,
Ndege wa angani, na samaki wa baharini,
Na kila kipitiacho njia za baharini. (K)
SHANGILIO
Ebr. 4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi
kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.
INJILI
Mk. 1:21-28
Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpka
Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.
Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akifundisha kama mtu
mwenye amri, wala si kama waandishi.
Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu
mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti?
Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu
akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa,
akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema,
Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao
wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya
Galilaya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment