MASOMO Y AMISA, JANUARI 15, 2023
DOMINIKA YA 2 YA MWAKA A WA KANISA
SOMO 1
Isa. 49:3, 5 – 6
Bwana akaniambia; Wewe u mtumishi wangu,
Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.
Na sasa Bwana sema hivi, yeye aliyeniumba tangu
tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee yakobo tena, na Israeli wakusanyike
mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu
wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa
mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli
waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu
wangu hata miisho ya dunia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 40:1, 3, 6 – 9 (K) 7, 8
(K) Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja,
kuyafanya mapenzi yako.
Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
Akatia wimbo mpya kinywani mwangu
Ndio sifa zake Mungu wetu. (K)
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
Nimehubiri habari za haki
Katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu;
Ee Bwana, unajua. (K)
SOMO 2
1Kor. 1:1 – 3
Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa
mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho,
wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote
wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu.
Neema na iwe kwenu na Amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu
Kristo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 12:13
Aleluya, aleluya,
Walisema, ndiye mbarikiwa, mfalme ajaye kwa jina
la Bwana,
Aleluya.
INJILI
Yn. 1:29 – 34
Siku ya pili Yohane Mbatizaji amwona Yesu
anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya
ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu;
ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua;
lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa
maji. Tena Yohane akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka
mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka
kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa
juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena
nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment