Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUBAKI DAIMA KWAKULITAZAMA FUMBO LA NOELI


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi, Januari 7, 2023

1 Yoh 5:14-21;
Zab 149: 1-6.9;
Yn 2:1-11


YESU ANATAKA KUTENDA MUUJIZA KWA AJILI YAKO 

Injili ya leo inatualika kwenye karamu. Harusi ya kawaida ya huko Kana inatumika leo kwa Yesu kuonesha Umungu wake na utakatifu wake kwa kubadilisha maji kuwa divai. Muujiza huu unatendwa kutokana na ombi la Mama kwa Mwanaye, unatendwa mbele ya Wafuasi wa kwanza wa Yesu. 

Injili ya Yohane ni Injili tofauti na Injili nyingine tatu. Lazima kuwa makini kuelezea kabla mtu hajahitimisha bila kuaelewa Lugha ya asili. Yohane daima yeye husisitiza juu ya asili ya Yesu kwamba ni Mbinguni na pia mamlaka yake na muungano na Baba yake. Yohane katika Injili hakumtaja Maria kwa jina. Lakini daima amempa heshima ya kumwita Mama wa Yesu. Katika nyakati zote amesisitizia juu ya uasili wake wa Mbinguni na matayarisho yake katika mateso, kifo na ufufuko. (Saa yake). 

Leo tunaweza kusema ni kama epifania ndogo, Yesu anaonesha utukufu wake. Yohane anauita ni muujiza au ishara yake ya kwanza. Anasema pia hii imetokea siku ya tatu, ishara pia ya siku ya ufufuko, alipo onesha utukufu wake. Yesu anafanya uumbaji upya kwa yeye mwenyewe kuwa divai mpya, ambapo itakuwa ni damu yake ya Agano Jipya kwa ajili ya kufanya upya ubinadamu. 

Leo mama Maria anatueleza kitu cha tunachotakiwa kufahamu: “tufanea kila anachotuambia”. Ni kitu gani tena tunahitaji kufahamu? Tunapaswa kutenda kadiri ya Injili kwani haya ndiyo Yesu aliyotuambia sisi. Tunaweza kuwaelekeza wengine alichosema Yesu na kutoa mifano mizuri, ila sisi wenyewe kulimwilisha neno hili na kuliweka katika maisha yetu imekuwa msalaba na hatupo tayari. Tunasikia raha tuu kuwahubiria wengine alichosema Yesu ila sisi hatujihubirii kwanza. Injili lazima ianze na wewe binafsi kabla haijaenda kwa wengine.: 

1) tunapaswa kutambua anachotaka Yesu na, 
2) na kukubali yote aliotuambia.  

Kutambua mapenzi ya Mungu inaweza kuwa ngumu wakati mwingine kwani tuna mambo mengi mno na tunashindwa kusikia ile sauti yake ya chini kabisa. Yeye halazimishi mtu kushika mapenzi yake, bali ni sisi kuyakubali kwa uhuru wetu na kuyatenda. Anatuhitaji tumpe akili na uwezo wetu wote. Yesu ameyaweka maneno yake wazi kiasi ambacho ametufundisha namna ya kuikataa dhambi na kufuata mapenzi yake, lakini ukweli ni kwamba bado hatujampa Yeye akili na fikra zetu zote atusaidie kuanza vyema. Tunaongozwa mno na hisia na mwazo yetu wenyewe. 

Pili, tunapaswa kufahamu pia wakati mapenzi ya Mungu yanapokuja kwetu sio rahisi sana kuyatambua na kuyafuata. Yanahitaji kila kitu kutoka kwetu. “Yeye ni Mungu mwenyewe wivu”. Hapendi unapomfuata uanza kuchanganyachanganya mambo. Anahitaji ujitoe kwa moyo wote bila kujibakiza. 

Leo, Mungu anahitaji kufanya miujiza katika maisha yako. Anahitaji wewe utambue mapenzi yake na kuyafuata, kunahitajika sadaka katika kufuata mapenzi haya. Anataka kubadili maisha magumu akupe utukufu. Je upo tayari? Upo tayari kuachana na yule mume wa mtu? Yule mke wa mtu upo tayari kuachana naye? Upo tayari kuacha kuchukua fedha kwa siri kutoka ofisini kwako? Upo tayari kuacha marafiki wabaya wanaokupeleka kwenye dhambi kila siku? Upo tayari kuondokana na mazingira ya dhambi yanayokudondosha kila siku? Kuwa jasiri omba neema uweze kupandishwa katika utukufu kwa kuacha dhambi. 

Ni lazima utambue udhaifu wako kwanza na hapo ndipo mapenzi ya Mungu yatatendeka vizuri sana katika maisha yetu. Wengi wetu tunakataa udhaifu wetu. Pia ni lazima tujiandae wenyewe katika sala na uvumilivu, wapo watu wanaokuchokoza ili uingie kwenye dhambi, kuwa makini usianguke na daima baki katika sala na taratibu utayagundua mapenzi ya Mungu na kuyatenda. Na daima yaoneshe mapenzi ya Yesu kwa njia ya upendo. 

Sala: Mama wa Mungu, tunakushukuru kwa meneno yako yenye hekima. Nisaidie mimi niweze kukubali ushauri wako katika maisha yangu. Nisaidie niweze kutambua Mwanao ananitaka nini mimi nitende. Yesu nakupa wewe maisha yangu na nachagua kujiweka kwako. Yesu nakuamini wewe. Amina.

Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment