“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatatu, Januari 30, 2023
Juma la 4 la Mwaka wa Kanisa
Ebr 11: 32-40;
Zab 31: 20-24;
Mk 5: 1-20.
KUBADILISHWA NA YESU!
Leo tunaona Yesu anakutana na mtu mwenye pepo wachafu wengi. 'Legioni' wa
mapepo anatambua nguvu na utakatifu wa Yesu, na anamsihi asiwapeleke nje ya
nchi ile. Yesu anawaamuru kwamba wao wamtoke mtu huyo na kwa nguvu ya Neno lake
waende kwenye kundi kubwa la nguruwe, kisha nguruwe waliokuwa gengeni
wakateremka kwa kasi, na kuzama katika bahari.
Katika injili ya Marko, Legioni (Jeshi) ni ishara ya Roma. Utakatifu wa
Yesu na nguvu, itakuwa kwaajili ya kuwakomboa wote waliofungwa na roho ya
dhambi. Mabaya hayawezi kusimama dhidi ya Yesu yatashindwa kwa ukweli na
mamlaka yake. Uchaguzi ni wetu kuwa huru au la. Wagerasi walimuomba Yesu
aondoke katika eneo lao kutokana na hofu ya nguvu zake. Yule aliyekombolewa
alikwenda sehemu mbalimbali, kueneza habari njema.
Je! wewe na mimi tukoje? Je! uko tayari kukombolewa au tunataka kumkataa
Yesu kama Wagerasi? Mungu ametupa utashi wakutambua mema na mabaya, ni juu yetu
kutumia uhuru wetu vizuri kuchagua lililo jema kwa manufaa ya roho zetu. Dhambi
ni matokeo mabaya ya matumizi ya uhuru aliotupa Mungu. Mungu kamwe haingilii
uhuru wetu, wakati mwingine tunaona mambo mengi mabaya yanatokea tunajiuliza
Mungu haoni kweli? Ukweli ni kwamba Mungu anaona lakini kamwe haingilii uhuru
wa mwanadamu aliompa anapenda sisi tutumie uhuru wetu vizuri tukijua mabaya na
mema, ili tuwe huru kuchagua kati ya hayo mawili. Tuombee neema yake ili
tumchague yeye aliye asili ya wema wote.
Sala: Bwana, ninafurahi katika nguvu zako za Kuu. Ninafurahiai katika ukuu
wako na utukufu wako. Nisaidie niweze kuona mara nyingi unapokuwa katika hali
mbalimbali ukitenda kazi ndani ya wote walio karibu yangu. Ninapo ona nguvu
yako ya kuokoa ikiwa katika kazi, jaza moyo wangu kwa shukrani kwa yote
unayotenda. Ninaomba Neno lako na mamlaka yako yafukuze yote yanayo niongoza
kwenye dhambi. Yesu nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment