Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

UNYENYEKEVU NJIA YA KUMPATA MUNGU!


“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Desemba 4, 2016.
Dominika ya 2 ya Majilio, Mwaka “A”

Isa11:1-10;
Zab 71:1-2, 7-8, 12-13, 17;
Rum 15:4-9;
Mt. 3:1-12.


UNYENYEKEVU NJIA YA KUMPATA MUNGU!


Katika Jumapili hii ya pili ya majilio, leo tunapewa Mt. Yohane Mbatizaji kama Zawadi. Ni zawadi ilioje! Yesu mwenyewe alisema kwamba Yohane Mbatizaji “kati ya wote walio zaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji” (Mt 11:11). Ni kitu ghani kinamfanya Yohane awe mkuu? Tunaweza kuona vitu viwili kwa pamoja. Cha kwanza ni, wito wake na cha pili ni fadhila yake. Yohane alikuwa mkuu kwasababu alikuwa nabii aliyekuwa katika mvusho wa kutoka Agano la Kale na kwenda Agano jipya. Alikuwa ni daraja la kuandaa maisha mapya yaliokuwa yanakuja. Utume wake wa pekee ulimfanya awe mkuu kweli. Lakini alikuwa mkuu si kwasababu tu ya utume wake wa pekee, bali alikuwa pia mkuu kwasababu ya fadhila alizokuwa nazo katika maisha. Ni zawadi hii inayo tufanya sisi tufikirie zaidi kuhusu hamu ya wokovu wetu kuliko yeyote yule. Fadhila ya pekee aliyo kuwa nayo Yohane Mbatizaji ni “unyenyekevu” kwani Yohane alikiri kwamba hastahili hata kulegeza Kamba za viatu vya Yesu (Mk 1:7). Aliendelea kusema kuhusu Yesu kwamba ‘ anapaswa Yesu azidi yeye apungue’ (Yn 3:30). Yohane hakuwako kwa ajili ya sifa na heshima bali alikuwako ili awaoneshe na kuwaelekeza watu kwa Yesu aliye Mkombozi wa Ulimwengu. Yohane alikuwa tayarii kutimiza utume wake na baadaye alijikabidhi kwa watesi wake. Unyenyekevu wake ulimfanya amuelekee Yesu tu na kutamani kuwaonesha watu wote kwake.

Majilio ni kipindi cha kusubiri ujio wa Masiha, lakini pia hata hivyo Bwana anatusubiri sisi tumrudie. Mungu wetu anatupenda, upendo wake unamfanya atutafute. Mungu alienda bustanini kumtafuta Eva na Adam, walipokuwa wakijificha, walijificha baada ya kushindwa kutii mapenzi ya Mungu. Sisi pia tunajificha mbele ya uso wa Mungu tunapoishi kinyume na mapenzi yake. Wakati mwingine tunalalamika Mungu amejificha mbele ya uso wetu. Na kwamba haonekani, wakati ukweli ni kwamba sisi ndio tuliojificha mbele ya uso wake! Na hapo Mungu akauliza swali “uko wapi? ” ni yeye aliyeanza kututafuta, kwasababu ya upendo wake kwetu. Katika hali zote katika Agano la kale Mungu amekuwa akimtafuta mwanadamu, na kutaka apokee tena upendo wake. Katika Injili ya leo Yesu anatutaka tutoke katika sehemu zetu tulipo jificha na kutembea naye tena. Je, tupo tayari kutoka njee? Je, tupo tayari kusafisha dhambi zetu nakurudi tena? Je, tutafanya juhudi ya kuachana na dhambi zetu ambazo tumesha fanana nazo? Tupo tayari kuwa watoto wa mwanga sasa?

Tutafakari sasa, juu ya unyenyekevu huu katika maisha yetu. Je, huwa tunajinyoshea vidole sisi au tunamuelekea Kristo? Je, tunatafuta sifa kwa wengine au tunaelekeza sifa zote kuwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu? Unyenyekevu ndio njia aliopitia Yohane Mbatizaji, sisi nasi tunapaswa kujitahidi kupitia njia hiyo kila siku. Tunaomba leo tuwe mashahidi wa unyenyekevu huku tukiwa katika njia sahihi ya kutekeleza mapenzi ya Mungu. Ni mioyo yetu tunayopaswa kuifanya iwe njia kuu ya kuelekea kwa Mungu. Ni bonde la dhambi katika mioyo yetu linalo paswa kujazwa na huruma ya Mungu na uponyaji. Ni milima na vichuguu vya majivuno vilivyopo ndani ya mioyo yetu vinavyopaswa kusawazishwa. Noeli itapoteza maana halisi kama hatutaiandaa mioyo yetu kuwa nia ya Bwana. Katika kipindi cha Majilio, tujiulize wenyewe, je, kuna dhambi yeyote inayonifanya nitengane na Mungu? Tutubu na kufanya maisha yetu kuwa mapya ili tuweze kukutwa vyema na Mungu wetu anaye tupenda.

Sala: Asante Bwana kwa kunisubiri na kunitafuta mimi. Nintamani kubaki katika pendo lako milele. Bwana, asante kwa zawadi ya Mt. Yohane Mbatizaji. Ninaomba ushuhuda wake wa unyenyekevu unisaidie mimi kutembea katika maisha yangu ya Kikristo. Nisaidie Bwana niweze kuwaelekeza watu kwako daima na sio kwangu. Yesu nakuamini wewe. Amina. 

                                     
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment