“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Desemba 20, 2022
Juma la 4 la Majilio
Isa 7: 10-14;
Zab 24: 1-6;
Lk 1: 26-38
MUNGU ANAFANYA VITU VYOTE VIWEZEKANE
Leo tunapewa ushuhuda wa Imani kamili na Mama
yetu Mbarikiwa. Jibu lake lilikuwa nini? “mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendwe
kama ulivyo nena.”. Katika hali ya mapokeo tunaongelea hili kama “NDIO” kuu
yake kwa Mungu. Kitu kimoja katika hili ni kwamba Mama yetu anajikabidhi kabisa
hata kabla hajaelewa. Malaika anatoa maelezo mafupi kwake, lakini ukitazama kwa
undani sio maelezo mafupi hayo yaliomfanya Mama Maria aamini. Alikuwa amesha
amini, na hivyo Imani ilikuwa inatafuta uelewa. Si kwamba alisikiliza maneno
haya na kuanza kuyachambua kama yanafaa au la! Alisikiliza, akayaweka moyoni na
mara moja akajitoa kwa maneno yaliyo zungumzwa. Imani ya mama yetu ilikuwa ni
Imani ile iliofahamu ukweli bila uelewa kamili.
Je, wewe na mimi tupo tayari kujikabidhi kwenye
mapenzi ya Mungu na ukweli bila kuelewa? Je, tunamuamini Mungu zaidi kuliko
tunavyo amini akili yetu ya kibinadamu? Je, tupo tayari kusonga mbele kwa Imani
zaidi kuliko kuamini akili zetu pekee? Tujitahidi kuiga akili ya Imani ya Mama
yetu. Aliujua ukweli kwasababu uliongelewa ndani ya moyo wake. Aliusikiliza na
kujitoa na kukumbatia mapenzi ya Mungu.
“Tazama, Bikira atachukua mimba na atamzaa Mwana
na jina lake utamwita Emmanueli”. Na Emanueli “Mungu pamoja nasi” hakuishi tu
katika sayari yetu kwa miaka elfu mbili iliopita, bali amebaki nasi tangu
daima. Kwa njia ya ubatizo Emanueli alizaliwa tena kwetu kwa maji na kwa Roho
Mtakatifu. Hatuwezi kupima upendo wa Kimungu unao msukuma Mungu wa milele
kuingia katika mioyo yetu midogo. Jibu letu linapaswa liwe kama la Maria.
Tunapaswa tujifungue wenyewe katika undani wa Kristo, tumruhusu Kristo abadili
mahusiano yetu mabaya, na kazi zetu mbaya.
Sala: Bwana, natamani kukuamini wewe kwa akili
yangu yote, moyo wangu wote na nguvu zangu zote. Nisaidie niweze kukusikia wewe
ukiongea niweze kujibu kwa Imani kamili na ukarimu. Bwana naomba niige Imani
kamili ya Mama yako kwa kusali daima naye, ‘naiwe kwangu kama ulivyo nena”.
Mama Maria, utuombee. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment