MASOMO YA MISA JANUARI 1, 2023
SHEREHE YA MARIA MTAKATIFU MAMA WA MUNGU
SOMO 1
Hes. 6:22-27
Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Nena na Haruni na wanawe, uwaambie,
Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; Bwana akubarikie, na
kukulinda; Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie
uso wake, na kukupa Amani. Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa
Israeli; nami nitawabarikia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 67:1-2,4,6-7 (K) 1
(K) Mungu na atufadhili na kutubariki.
Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)
Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)
Nchi imetoa mazao yake;
Mungu, Mungu wetu, ametubariki.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)
SOMO 2
Gal. 4:4-7
Ndugu zangu: ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye
amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao
waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa
kuwa ninyi mmekuwa wana. Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye,
Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana na kama u
mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
INJILI
Lk. 2:16-21
Siku ile: Wachungaji wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na
yule mtoto mchanga amelala horini. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu
ya huyo mtoto. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na
wachungaji. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.
Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote
waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa. Hata zilipotimia siku nane za
kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla
hajachukuliwa mimba.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment