MASOMO YA MISA DESEMBA 5, 2022
JUMATATU, JUMA LA 2 LA MAJILIO
SOMO 1
Isa. 35:1-10
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa
litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi,
naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na
Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu.
Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti
yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama,
Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.
Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi
yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake
aliye bubu utaimba; maana katika maji yatabubujika; na vijito jangwani.
Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na
nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa
wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.
Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia
ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu
hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo. Hapo
hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo;
bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.
Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni
wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko
na furaha, huzuni na kuugua zitamkimbia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 85:8-13 (K) Isa. 35:4
(K) Tazama Mungu wetu atakuja na atatuokoa.
Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake Amani.
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Tazama Mfalme, Bwana wa ulimwengu, Yeye ataiondoa nira ya
utumwa wetu.
Aleluya.
INJILI
Lk. 5:17-26
Ikawa siku zile, Yesu alikuwa akifundisha, na Mafarisayo
na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha
Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya.
Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu wmenye
kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi
ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari
wakampitisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati
mbele ya Yesu. Naye alipoiona Imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa
dhambi zako.
Basi, wale waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana
wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? N’nani awezaye kusamehe
dhambi isipokuwa Mungu peke yake? Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia,
Mnahojiana nini mioyoni mwenu? Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa
dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa
Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwmbia yule mwenye kupooza).
Nakuambia, Ondoka, ujitike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. Mara
hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani
mwake, huku akimtukuza Mungu.
Ushaangao ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa
hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment