“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumanne, Desemba 3, 2024
Juma la 1 la Majilio
Kumbukumbu ya Mt. Fransisko Ksaveri (Padre).
Isa 30: 19-21, 23-26;
Zab 147: 1-6;
Mt 9:35 - 10: 1, 6-8
KUISIKILIZA SAUTI YA MUNGU!
Katika somo la kwanza tunasikia: hata kama
tukigeuka kulia, au kushoto, tutaisikia sauti nyuma yetu ikisema “Njia ni hii,
ifuateni”, Nabii Isaya anawahakikishia
watu kuwa kama watatafuta muongozo wa Mungu, watalipata jambo hili – “Njia ni
hii, ifuate!”
Leo tuna adhimisha kumbukumbu ya Mt. Fransisko
Ksaveri, msimamizi wa Misioni (utume). Hari yake ya kimisionari ya kuhubiri
Injili ilimpeleka India, Japan na China. Mt. huyu alisikia sauti ya Mungu
kupitia Mt. Inyasi ‘yamfaa mtu nini kuupata ulimwengu mzima lakini akapoteza
roho yake?’ hapa Fransisko alijisikia kulazimika kusikiliza. Na hili lilimfanya
“ahubiri Injili kama kazi yake na kujitoa” Fransisko alijisikia mwenye nguvu
kwasababu alijiaminisha kwa Mungu na ndani ya Kristo.
Hatutakuwa huru kamwe mpaka pale tutakaposikia na
kuitii sauti ya Mungu. Ni juu yetu kuweka vema akili zetu kuyakubali mapenzi ya
Mungu kwa ajili ya maisha yetu, bila kujali ni kitu gani! Sisi sote tunakosea
hapa na pale katika maisha. Baadhi yetu tunakosa muelekeo njiani na kukata
tamaa. Sisi hatupaswi kukata tamaa tunapaswa kujipanga tena vizuri na kutilia
maanani sauti ya Mungu ndani yetu na kuifuata.
Sala: Bwana, ninakushukuru kwa zawadi ya maisha.
Asante kwa kuja duniani na kuingia katika maisha yangu. Asante kwa furaha ya kukufahamu
wewe na kukupenda wewe. Ninaomba nikuruhusu ubadili maisha yangu niendelee
kukutafuta wewe na kukuonesha kwa wengine. Yesu, nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment