MASOMO YA MISA NOVEMBA 9, 2022
JUMATANO, JUMA 32 LA MWAKA WA KANISA
SIKUKUU YA KUTABARUKIWA BASILIKA LA LATERANI
SOMO 1
Eze. 43:1-2, 4-7
Malaika alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile
lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli
ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji
mengi, nayo nchi iling’aa kwa utukufu wake. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia
ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha
Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana
uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo;
na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti
changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa
Israeli milele.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SOMO 2
1Kor. 3:9-11, 16-17
Ninyi ni jingo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu
niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu
mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu
yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule
uliokwisha kuwekwa, yaani, yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi
huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani, au manyasi, kazi
ya kila mtu itakuwa Dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa
katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani.
Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, nay a kuwa
Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu
atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1-7 (K)
(K) Tuje mbele za Bwana kwa shukrani.
Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,
Na mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Mkononi mwake zimo bonde za dunia,
Hata vilele vya milima ni vyake.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya,
Na mikono yake iliiumba nchi kavu. (K)
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
SHANGILIO
2 Nya. 7:16
Aleluya, aleluya,
Nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, asema Bwana, ili
kwamba jina langu lipate kuwako huko milele.
Aleluya.
INJILI
Yn. 2: 13-22
Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu alikwea
mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo
na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa
wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja
fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni
haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake
wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila.
Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani
utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu
hili, name katika siku t atu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu
hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha
katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi
alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi,
wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment