MASOMO YA MISA, NOVEMBA 22, 2022
JUMANNE, JUMA LA 34 LA MWAKA WA KANISA
KUMBUKUMBU YA MT. SESILIA (Bikira na Shahidi)
SOMO 1
Ufu. 14:14 – 19
Mimi, Yohane, niliona, na tazama, wingu jeupe, na juu ya
wingu hilo ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya
kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka
katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa ameketi juu ya lile
wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno
ya nchi yamekomaa. Na yeye aliyeketi juu ya wingu akautupa mundu wake juu ya nchi,
nchi ikavunwa.
Kisha malaika mwingine akatoka katika lile hekalu
lililoko mbinguni, yeye naye ana mundu mkali. Na malaika mwingine akatoka
katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti
kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundu wako mkali, ukachume
vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sansa. Malaika yule
akautupa mundu wake hata nchi, akauchuma mzabibu wa nchi, akazitupa zabibu
katika shinikizo hilo kubwa la ghadhabu ya Mungu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 96:10 – 13 (K) 13
(K) Bwana atauhukumu ulimwengu kwa haki.
Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili.
Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo. (K)
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
SHANGILIO
Yak. 1:21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu, lililopandwa ndani,
liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.
INJILI
Lk. 21:5-11
Watu wa kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu,
jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, Yesu alisema, Haya
mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo
halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo
ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia?
Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi
watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi
msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana,
hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha
aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme;
kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na
mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment