Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, NOVEMBA 16, 2022


MASOMO YA MISA, NOVEMBA 16, 2022
JUMATANO, JUMA LA 33 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Ufu. 4:1 – 11

Mimi, Yohane, niliona mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti; na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.

Na viti ishirini na vine vikilizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wane, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu. Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto ziliwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.

Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wane, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa Mwanadamu; na mwenye uhai wan ne alikuwa mfano wa tai arukaye.

Na hawa wenye uhai wane, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.

Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wane huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 150 (K) Ufu. 4:8

(K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi.

Aleluya.
Msifuni Mungu katika patakatifu pake,
Msifuni katika anga la uweza wake.
Msifuni kwa matendo yake makuu;
Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake. (K)

Msifuni kwa mvumo wa baragumu;
Msifuni kwa kinanda na kinubi;
Msifuni kwa matari na kucheza;
Msifuni kwa zeze na filimbi. (K)

Msifuni kwa matoazi yaliayo;
Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.
Aleluya. (K)



SHANGILIO
Yn. 8:12

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.



INJILI
Lk. 19:11 – 28

Makutano waliposikia, Yesu aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana fungu lako limeleta mafungu matano faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

Akaja mwingine akasema, Bwana hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso, Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi, Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho.

Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwanchinje mbele yangu.

Na laipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment