MASOMO YA MISA, NOVEMBA 11, 2022
IJUMAA, JUMA LA 32 LA MWAKA WA KANISA
KUMBUKUMBU YA MT. MARTIN WA TOURS (ASKOFU)
SOMO 1
2Yoh. 1:4 – 9
Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako
wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba. Na sasa, mama,
nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu
mwanzo, kwamba tupendane.
Na huu ndio upendo; tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii
ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo.
Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri
ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga
Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu
timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye
hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119:1 – 2, 10 – 11, 17 – 18 (K) 1
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote. (K)
Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi. (K)
Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:28, 33
Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe
njia ya amri zako.
Aleluya.
INJILI
Lk. 17:26-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku
za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila
na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika
safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa
katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza,
wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na
kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku
ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.
Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo
ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee
nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu yeyote atakaye kuiponya nafsi yake,
ataiangamiza; na yeyote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu
wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia. Ulipo
mzoga, ndipo watakapokutanika tai.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment