Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, IJUMAA, NOVEMBA 4, 2022


MASOMO YA MISA, IJUMAA, NOVEMBA 4, 2022
JUMA LA 31 LA MWAKA WA KANISA

Kumbukumbu ya Mt. Karoli Borromeo, Askofu.


SOMO 1
Flp 3:17—4:1

Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.

Neno la Bwana
Tumshukuru Mungu.




WIMBO WA KATIKATI
Zab 122:1-5

(K) Nalifurahi walipo niambia, na twende nyumbani kwa Bwana

1. Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.(K)


2. Ee Yerusalemu uliyejengwa Kama mji ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila, Kabila za Bwana; (K)

3. Ushuhuda kwa Israeli, Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi.(K)



SHANGILIO                              
Yn 14:23

Aleluya, aleluya
Mtu akinipenda, atalishika neno langu,
na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake.
Aleluya




INJILI
Lk. 16:1-8

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena. Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda, ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.

Akawaita wadeni wa bwana wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema, Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini. Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano. Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.

Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment