Alhamisi, Novemba 3, 2022,
Juma la 31 la Mwaka wa Kanisa
Flp 3:3-8;
Zab 104:2-7;
Lk 15:1-10
KUPOTEA NA KUPATIKANA!
Je ni ujumbe ghani anaotaka kutuambia Yesu kuhusu Mungu na ufalme wake
katika mfano wa kondoo aliyepotea na shilingi iliyopotea? Wote wawili,
Mchungaji na Mama mwenye nyumba, “wanatafuta mpaka wapate kilicho potea”.
Wanatafuta bila kukata tamaa. Jambo jipya analotaka kutufundisha Yesu ni kwamba
wadhambi ni lazima watafutwe warudi sio kuwaombolezea. Mungu hafurahii kupotea
kwa mtu yeyote, bali anatamani wote wakombolewa wawe na uhusiano naye tena.
Ndio maana jumuiya yote ya Mbinguni hufurahi juu ya mwenye dhambi mmoja
anapopatikana na kurudisha uhusiano wake na Mungu kwa kutubu. Watafuta roho za
waliopotea leo hii wanahitajika sana. Je, tunasali bila kuchoka na kutafuta
kuwarudisha waliopotea katika njia ya kumwelekea Mungu? Au tunafurahia kupotea
kwa mwenzetu? Kushindwa kufurahia mafanikio ya wenzetu ni dhahiri kwamba
tunafurahia upande mwingine wa kupotea kwake. Daima tujifunze kuwarudisha watu
kwa Mungu, tuwaombee na kuwatia moyo ili sote tushikane mikono tuende kwa
Mungu.
Sala: Bwana, naomba mwanga wako uondoe giza ili kile kilichopotea
kipatikane. Nijaze kwa upendo wako wakubadilisha mioyo yetu ili niweze kuwa na
huruma kama wewe ulivyo na huruma. Amina.
No comments:
Post a Comment